Serikali yaonya madereva bodaboda

14Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yaonya madereva bodaboda

SERIKALI imewaonya madereva wa bodaboda wanaoshiriki matendo ya uhalifu ikiwamo usafirishaji wa wahamiaji haramu, dawa za kulevya, mauaji na uporaji wa vitu kuwa atayekamatwa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yalisemwa jana jijini Arusha na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo, wakati wa kikao maalumu kilichowashirikisha madereva wa bodaboda, daladala na bajaji kujadili mambo mbalimbali ikiwamo ushiriki wa bodaboda kwenye matukio ya uhalifu na kuzidisha abiria katika vyombo hivyo.

Chilo aliwaambia madereva hao kuwa taifa linawategemea kama nguvu kazi.

“Nawaasa bodaboda kuachana na matendo ya kihalifu, serikali tunawategemea sana vijana kama nguvu kazi, lakini kuna baadhi ya vijana siyo wote wanatumika katika matukio ya uhalifu ikiwamo ujambazi, dawa za kulevya na wengine wakitumika huko mipakani kusafirisha wahamiaji haramu sasa tusizitumie bodaboda zikaleta sura mbaya kama chombo cha kutumika kufanya uhalifu wakati lengo lake ni kutumika kujikwamua kiuchumi,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, aliwaomba bodaboda kutii sheria za usalama barabarani huku wakisubiri mapendekezo ya Bunge kuhusu kila kosa kutozwa Sh. 10,000 kupitishwa.

“Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha kushushiwa gharama ya faini kutokana na makosa ya barabarani, tunamshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kusikia kilio chenu nawaomba sasa mfuate sheria za usalama barabarani mkishirikiana na Jeshi la Polisi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Justine Maseji, aliwaonya watu wanaoshiriki matendo ya kuteka na kuwaua madereva bodaboda huku akielezea kuwa yeyote anayejaribu kucheza na maisha ya Watanzania atashughulikiwa.

“Mpaka mwezi wa tatu tumekamata pikipiki 60, nitoe onyo kali kwa watu wanaopora mali za wananchi waache kufanya mambo ya ovyo ovyo tutachukua hatua kali, mtu anayetafuta dozi sisi tutapeleka dozi kali zaidi na wao wahalifu wanafahamu maana sio kila kitu tunaweka wazi wanazijua ‘sindano’ tunazopeleka,” alisema.

Habari Kubwa