Siku 30 kuamua hatima kigogo wa IPTL

26Feb 2021
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Siku 30 kuamua hatima kigogo wa IPTL

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa siku 30 kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na mmiliki wa Kampuni ya  Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Habinder Seth pamoja na Mwanasheria wa kampuni hiyo,  Joseph Mwakandege, kukamilisha mchakato wa....

makubaliano ya kumaliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Hata hivyo, Mahakama hiyo imesema DPP ana mamlaka ya kukubali au kukataa maombi yanayowasilishwa kwake ikiwamo  kuingia kwenye makubaliano ya kumaliza kesi na washtakiwa, na kwamba halazimishwi  kufanya hivyo kisheria.

Amri hiyo ilitolewa jana katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Awali, wakili wa utetezi, Melchisedeck Lutema na Mwakandege waliwasilisha malalamiko yao kuwa wateja wao wamemwandikia DPP barua ya kuomba kufanya makubaliano zaidi ya mara mbili, lakini hawajapata majibu.

Wakili Lutema alidai kuwa mteja wake alimwandikia DPP barua Julai Mosi, 2019 na ilipokolewa ofisini kwake Julai 23, 2019, barua ya pili Seth aliiandika Julai 20, 2020 na kupokelewa Septemba 10, 2020 bila majibu.

Aidha, alidai utetezi unaifahamisha mahakama kuwa mteja wake yuko tayari kuingia makubaliano na DPP ya kumaliza kesi na pia kwa mujibu wa Kanuni ya 3 ya makubaliano mapya zilizotolewa na Jaji Mkuu mwaka 2021, chini ya Kifungu cha 5 cha kanuni hizo, mahakama ina mamlaka ya kutoa muda kwa pande husika kujadiliana na kukamilisha makubaliano ya kumaliza kesi kwa muda wa siku 30.

"Mheshimiwa hakimu, tunaomba siku 30 ili tuendelee na mchakato na DPP,” Lutema aliiambia mahakama.

Aliendelea kudai kuwa Juni 2, 2021 Sethi aliiandikia mahakama hiyo barua ya malalamiko na kupokelewa Februari Mosi, 2021, kuwa hakuletwa mahakamani ndani ya miezi saba.

Alidai kuwa hayo yote yamekuwa yakifanyika bila sababu yoyote, licha ya kuwa  ni takwa la kisheria mahabusu kuletwa mahakamani  ndani ya siku 14, kwa hiyo anaomba safari ijayo mteja wake aletwe mahakamani.

Kwa upande wake, Sungwa aliieleza Mahakama kuwa mteja wake (Mwakandege) aliandika barua Januari 8, 2021, kwa DPP akiomba makubaliano ya kumaliza kesi, hivyo kuiomba Mahakama itoe maelezo.

Akijibu homa hizo, Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah, alidai katika suala la kutokuletwa mahakamani katika  kumbukumbu zake mara ya mwisho kuletwa mahakamani ilikuwa Desemba 17, 2020 kwa hiyo si kweli kuwa miezi saba hawakuletwa mahakamani.

"Ni kweli sheria inataka ndani ya siku 14 washtakiwa waletwe mahakamani na pale ambapo tumeshindwa kuwaleta tunatoa sababu na kuonyesha kwamba kuwa hatuma nia mbaya… wamekuwa wakiomba ahadi ya kuwaleta mahakamani, kwa hiyo hakuna haja ya mahakama kutoa amri hiyo tena," alidai Ngukah.

Kuhusu suala la makubaliano, Ngukah alidai kwa sababu mahakama imeshapewa taarifa, utaratibu ufuatwe uliyoelekezwa kisheria, lakini yeye hana barua ambazo walizizungumzia.

"DPP ana mamlaka kisheria ya kuingia makubaliano au la, hawezi kulazimishwa kuingia kwenye makubaliano,” alidai.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shaidi alisema kuhusu suala la washtakiwa kutokuletwa mahakamani, sheria iko wazi hivyo ifuatwe, ndani ya siku 14 waletwe mahakamani.

"DPP ana mamlaka ya kukubali au kukataa kuingia kwenye makubaliano na halazimishwi, lakini sio kukaa kimya kwa kuwa Jaji Mkuu ameshatoa kanuni mpya, ambazo zinaelekeza mahakama kutoa maelekezo.

"Basi hilo lifanyike ndani ya siku 30 kuanzia leo (jana), na kesi itakuja tena kwa kutajwa Machi 11, 2021,” alisema Hakimu Shaidi.

Mbali na Seth na Mwakandege, mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara, James Rugemalira, ambao wanakabiliwa na mashtaka  12.

Miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Makandege, anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000.

Habari Kubwa