TCRA kufungia laini zisizosajiliwa kwa mfumo mpya

16Apr 2019
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
TCRA kufungia laini zisizosajiliwa kwa mfumo mpya

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kuwa itawafungia laini zao za mawasiliano wale wote watakaoshindwa kuzisajili kwa mfumo mpya wa alama za vidole (Biometric Registration).

Afisa wa mawasiliano kutoka TCRA kanda ya ziwa Maria Katula akitoa maelekezo juu ya mfumo mpya wa usajili wa laini kwa njia ya vidole kwa wananchi wa Bariadi. picha happy severine.

Mamlaka hiyo imesema kuwa muda wa ukomo utakapotangazwa hakutakuwa na msamaha wowote na badala yake watazifungia mawasiliano laini zote zitakazokuwa hazijasajiliwa kwa mfumo huo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa mamlaka hiyo kanda ya ziwa Mhandisi Francis Mihayo, katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya mfumo huo uliofanyika mjini Bariadi mkoani Simiyu.

Mihayo alisema kuwa usajili wa laini zote kwa mfumo huo utaanza rasmi Mei 1, 2019, na wananchi watatakiwa kwenda kwa watoa huduma wa mitandao mbalimbali ya simu kwa ajili ya kusajiliwa.

Aidha amesema kuwa lengo la TCRA kuja na mfumo huo ni kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi waliosajili laini kwa kutumia vitambulisho feki.

Akizundua kampeni hiyo mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kusajili laini zao upya kwa mfumo huo, huku akiwataka kwenda na vitambulisho vya NIDA.

Aidha Kiswaga aliwataka wadau mbalimbali wa mawasiliano nchini kuunga mkono jitihada za utendaji kazi wa TCRA kwa kufuata maelekezo yanatolewa ili kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kimitandao.

Habari Kubwa