Ulimwengu ataja umuhimu Katiba mpya

18Oct 2021
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Ulimwengu ataja umuhimu Katiba mpya

WATANZANIA wamehamasishwa kupaza sauti zao kudai Katiba mpya ambayo itasaidia kukidhi mahitaji yao na kuongeza uwajibikaji baina ya viongozi na wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mwandishi mkongwe nchini, Jenerali Ulimwangu, wakati wa mdahalo wa kufanya uchambuzi wa Rai ya Jenerali Juzuu ya tatu iliyokuwa na mada isemayo Miaka 25 ya Rai ya Jenerali Demokrasia na Ukuu wa Katiba Tanzania uliofanyika jijini hapa.

Alisema madai ya Katiba Mpya sio matakwa ya wanasiasa bali ni ya kila mwananchi kwa umuhimu huo kila mmoja ashiriki kudai ili upatikane kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

“Mimi ni muumini wa haki ambayo kwa utashi wangu na ukongwe wangu, naamini ili tupige hatua na kuongeza uwajibikaji Katiba Mpya ni suluhisho, tushirikiane bila kujali itikadi za kisiasa, dini wala rangi kwa sababu katiba itamnufaisha kila mwananchi,” alisema Ulimwengu.

Alisema maandiko mengi aliyoanza kuandika tangu enzi za Hayati Mwalimu Nyerere hadi sasa yanalenga kuhimiza utawala bora na sheria ili kila mmoja awajibike kwa nafasi yake.

Aliwaonya wananchi kuwa makini na baadhi ya wanasiasa ambao wanapohitaji madaraka hunyenyekea na kutoa zawadi na wanapopata madaraka hutoa mabawa.

Miongoni mwa washiriki wa mdahalo huo ambao uliwahusisha pia Kituo cha Haki za Binadamu nchini (LHRC), Ofisa Programu wa Kituo hicho, Tito Magoti alisema Katiba Mpya itakuja na suluhisho na kuhakikisha usalama kwa wananachi wanaotoa maoni kwa lengo la kuboresha serikali.

Alisema Katiba Mpya inafukia mashimo yote yanayoonekana sasa na itasaidia wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao kujipatia maendeleo.

Aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), alimpongeza Jenerali Ulimwengu kwa kuanzisha mdahalo huo nchini na kwamba kwa kuwa tayari mchakato wa Katiba mpya ulianza ni vyema sasa kura zikaanza kupigwa ili kuipitisha katiba hiyo.

Alisema ni fedha nyingi zilitumika katika mchakato huo ambao ulizingatia mahitaji ya wananchi na kutolewa kwa maoni kinachohitajika ni kuanza kwa utaratibu wa kupiga kura kwa wananchi ili kuipitisha ianze kutumika.

Baadhi ya wananchi akiwamo Felister Kaisi, Mkazi wa Nsalala mjini Mbalizi alisema wananchi wasiogope kupaza sauti kudai haki kwa sababu wanatimiza haki yao ya kikatiba. Alisema baadhi ya viongozi wakipata madaraka wanajisahau na wanapokumbushwa huwa wakali na kuwadharau wananchi jambo ambalo alidai halikubaliki.

Habari Kubwa