Vodacom yajivunia mtandao kupanuka

25Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Vodacom yajivunia mtandao kupanuka

KWA kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Kampuni ya Vodacom Tanzania imepanua eneo la mtandao wake, katika maeneo ya vijijni na kuwafikia asilimia 92 ya wananchi na hivyo kujihakikishia nafasi yake ya uongozi katika utoaji wa huduma za mawasiliano nchini.

Uongozi wa kampuni hiyo, umebainisha kuwa teknolojia na uunganishwaji kimtandao, vina uwezo mkubwa wa kujenga jamii yenye usawa na ushirikishwaji kwa kuwezesha upatikanaji wa mtandao wa intaneti, ambao  unawezesha ushiriki kiuchumi.

Kampuni hiyo pia, imejiwekea lengo la kufikisha uunganishwaji wa mtandao kwa kasi ya broadband kwa asilimia 65 ya wananchi, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na lengo la mwisho ni kufikia asilimia 90, ifikapo mwaka 2024.

Hatua hii pia inaendana na lengo la serikali lililotangazwa la kuongeza uunganishwaji wa mtandao wa broadband kutoka asilimia 45 hadi kufikia asilimia 80. Hadi sasa, eneo lililounganishwa na Vodacom linawafikia asilimia 52 ya wakazi walio katika vijiji 1,184, nchini.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa kampuni hiyo kwa vyombo vya habari jana, ilibainisha kuwa kwa zaidi ya miaka 20, Vodacom Tanzania imekuwa ikiendelea kuwekeza na kuboresha mtandao wake, ili kuhakikisha kuwa inatoa huduma bora kwa wateja wake na kuwapatia teknolojia mpya na bidhaa za ubunifu.

Kutokana na uwekezaji huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 171.4, kwenye teknolojia ya 4G peke yake na kwamba Vodacom ina minara zaidi ya 3,000 yenye uwezo wa 2G, zaidi ya 2,800 ya 3G na zaidi ya minara 2,000 ya 4G.

Mkakati na sera za serikali ni zaidi ya kuwa na mtandao mpana tu bali kuhakikisha kuwa upatikanaji wa huduma hiyo ni wa haki na usawa kwa watu wake.

Upana wa mtandao wa Vodacom unaofikia maeneo yote ya nchi pia ni msingi wa utoaji wa huduma zinazookoa maisha kwa watumiaji walioko vijijini.

"Kwa ushrikiano na Hospitali ya CCBRT kwa mfano, zaidi ya wagonjwa 6,000 wa fistula wamepata huduma za upasuaji, wengi wao wakiwa wametokea vijijini," ilibainishwa katika taarifa hiyo.

Katika kuelekea kwenye jamii ya kidigitali, Vodacom Tanzania imejenga mtandao wa data wa kitaifa wenye kasi na wenye kuaminika unaowapatia watumiaji huduma za intaneti na kuongeza ushirikishwaji kwa jamii zilizotengwa na hata kusaidia kupunguza makali yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Yote haya, ikiwa vilevile ni kampuni inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha ulipaji kodi katika sekta nzima ya mawasiliano, ambapo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 ililipa Sh. trilioni 1.9, ikiwa ni kodi kwa serikali," ilibainisha zaidi katika taarifa hiyo.

Habari Kubwa