Wakurugenzi waliokopa benki biashara kitanzini

29Nov 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wakurugenzi waliokopa benki biashara kitanzini

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ametoa siku saba kwa wakurugenzi wa halmashauri kuwasilisha taarifa za mikopo waliyochukua benki za biashara baada ya utaratibu huo kupigwa marufuku na serikali.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, picha mtandao

Jafo ameonya kuwa mkurugenzi yeyote atakayeshindwa kuwasilisha taarifa sahihi za mikopo hiyo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, waziri huyo alisema baada ya kuwasilishwa taarifa hizo, ofisi yake itafanya tathmini na ikibainika kuna mkopo ulichukuliwa na kuna sura ya shaka, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

“Tunataka mkurugenzi wa halmashauri awasilisishe taarifa ya mikopo aliyochukua na kwa ajili gani, na riba yake ni kiasi gani, ndani ya wiki moja nipate taarifa katika halmashauri zote, sitegemei mkurugenzi yeyote afiche taarifa kuhusu halmashauri yake na endapo itabainika, hatua zitachukuliwa,” alisema.

Waziri Jafo pia aliziagiza halmashauri zilizochukua mikopo hiyo na bado hazijaanza kuitumia, zirejeshe fedha hizo katika taasisi husika za kifedha zilikokopa.

“Wale ambao wameshachukua mikopo ndani ya wiki hiyo moja ambayo wameshatumia, walete taarifa Tamisemi mikopo hiyo ina sura gani, ilikuwaje na ofisi yangu itatoa maelekezo katika mikopo hiyo ambayo imechukuliwa,”alisema.

Jafo alisema kuanzia jana, kila kitu kinasimama kuhusu mambo ya mikopo kama ambavyo Waraka wa Serikali unaelekeza.

“Halmashauri mbalimbali zimeonekana kuchukua mikopo kwenye benki za kibiashara kwa ajili ya miradi mbalimbali, jambo hili Rais jana (juzi) alilitolea maelekezo na alirejea kwamba halmashauri zilishaelekezwa kwa barua ya Desemba 13, 2016 yenye kumbukumbu namba CBC.155/233/01.”

“Barua ilizitaka taasisi zote za serikali, zikiwamo mamlaka za serikali za mitaa, hazipaswi kuchukua mkopo wowote kutoka katika benki ya kibiashara hadi pale serikali itakapojiridhisha.

"Katibu Mkuu Hazina atajiridhisha kuhusu mkopo huo, lakini hapa katikati imeonekana kuna baadhi ya halmashauri kupitia mabaraza ya madiwani, wamekaa vikao na wanaamua kuchukua mikopo,” alisema.

Alimwagiza Katibu Mkuu Tamisemi awasimamie wakurugenzi wake wote kuzingatia maelekezo ya serikali.“Jambo hili halitavumilika, Katibu Mkuu ahakikishe wakurugenzi hawafanyi mambo kinyume cha maelekezo ya serikali.

“Kama vile jana mlivyoona Halmashauri ya Kahama, Jiji la Arusha walitaka kukopa kwa ajili ya stendi na tayari tumezuia tangu wiki iliyopita, na halmashauri zingine nataka watii maelekezo," aliagiza.

Waziri Jafo alisema baada ya tathmini ya taarifa hizo, atatoa taarifa ya halmashauri zitakazokuwa zimebainika kukopa bila kufuata utaratibu.

“Sasa, inawezekana walikuwa wana nia njema, lakini jambo hili ni kinyume cha taratibu na maelekezo ya serikali, kutokana na suala hili nimeamua kutoa maelekezo kwa halmashauri zote nchini kuwa hazipaswi kuchukua mikopo ya aina yeyote katika benki za kibiashara," alisema.