Wanawake Wilayani Longido wakosa huduma za uzazi

19Sep 2021
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe Jumapili
Wanawake Wilayani Longido wakosa huduma za uzazi

WANAWAKE katika Kitongoji Cha Sokonoi Kijiji Cha Lumbwa kata ya Gelailumbwa tarafa ya Kitumbeine wilayani Longido Mkoa wa Arusha hawahudhurii kliniki ya mama na mtoto wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua kutokana na umbali wa kufuata huduma za afya.

Mwakilishi wa wanawake Naini Lukumay alisema kukosekana kwa huduma za afya kwenye eneo hilo hupelekea wakinamama kujifungua kwa njia isiyokuwa salama .

Alisema vifo vya mama na mtoto vinaweza kutokea kwani hawana wataalamu kutokana na kukosekana kwa Vituo vya afya katika eneo la jirani , makao makuu ya wilaya ni umbali wa kilomita 90 na kufika makao makuu ya Kijiji ni kilomita 25.

" Magonjwa ni mengi wanawake tunakosa huduma muhimu za uzazi na kupelekea mateso kwa jamii,tunamuomba Mama yetu Rais Samia atuangalie tuweze kupata kituo Cha afya" aliomba.

Akizungumza na Nipashe Mwenyekiti wa Kijiji hicho Richard Mollel,alisema wakinamama wanatembea umbali zaidi ya kilomita 25 kufuata huduma za uzazi hivyo kutokana na umbali huo,huwapelekea kutohudhuria kliniki hali ambayo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.

"Kukodisha  pikipiki hadi kufikia huduma ya afya nauli ni shilingi  30000 bado ni gharama zaidi" alisema Richard.

Alisema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 kitongoji hicho kilikua na jumla ya wakazi 1,168, hakuna huduma ya afya hivyo wananchi kwa ujumla wapo katika hatari ya kukosa matibabu na wakati mwingine vifo visivyo tarajiwa kwa kukosa huduma za afya hujitokeza.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri  Lankoi Olenini alisema wakati taratibu za kuanza kutumia zahanati hiyo zikiendelea kumalizika , halmashauri itaangalia namna ya kuanza kutoa huduma ya mobile clinic ili wananchi wapate haki yao ya matibabu ikiwemo wajawazito na watoto.