Wasomi wamlilia Profesa Luhanga

19Sep 2021
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Wasomi wamlilia Profesa Luhanga

VIONGOZI na wasomi wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Matthew Luhanga, aliyefariki dunia Jumatano.

Prof. Luhanga, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mzumbe, alifariki dunia mkoani Dar es Salaam wakati akiendelea na matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo alisema Profesa Luhanga alikuwa profesa mahiri katika eneo lake na wakati akiwa Rais wa Chama cha Wanafunzi wa UDSM, yeye alikuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho na aliwalea vizuri.

"Alitulea na kutuelekeza na ni mtu ambaye alikuwa anavumilia sana, aliruhusu mijadala, aliwaruhusu vijana kubishana naye bila changamoto yoyote na mwisho wa siku aliwaelekeza,” Prof. Mkumbo alisema.

Waziri wa zamani, Prof. Mark Mwandosya, akimzungumzia Prof. Luhanga, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, akisema: "Jua limezama leo jioni. Profesa Matthew Laban Pimpa Luhanga, ndugu na rafiki wa karibu, mwanafunzi mwenzangu, profesa mwenzangu, mhandisi mwenzangu, mwandishi mwenza, jirani yangu, ametutoka. Hatunaye tena. Mwenyezi Mungu amrehemu (RIP)."

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. William Anangisye, katika salamu zake za rambirambi, alisema wamepokea kwa masikitiko kifo cha Prof. Luhanga.

Prof. Anangisye alibainisha kuwa Prof. Luhanga alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 2006.

RATIBA YA MAZISHI

Msemaji wa Familia, Nehemiah Mchechu, aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), alisema jana kuwa maziko ya Prof. Luhanga yanatarajiwa kufanyika Jumanne katika makaburi ya Kwa Kondo, Tegeta mkoani Dar es Salaam.

"Jumatatu (leo) kuanzia saa nne asubuhi Jumuiya wa Chuo Kikuu itapata wasaa wa kuaga mwili shughuli ambayo itafanyika Ukumbi wa Nkrumah, (ratiba) ambayo itakwenda sambamba na misa maalum itakayofanyika katika kanisa la Chuo Kikuu (Charplain) na baadaye jioni kuanzia saa 12 ibada ya faraja itafanyika nyumbani kwa marehemu,” alisema.

Mchechu alisema kuwa Jumanne kuanzia saa 6:30 mchana misa pamoja na shughuli za kutoa heshima za mwisho itafanyika katika Parokia ya Mt. Andrea Mtume, Bahari Beach na kuanzia saa 10 jioni msafara utaelekea mkaburini kwa ajili ya maziko.