Waziri amkosoa Makonda taarifa mgonjwa corona

27Mar 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Waziri amkosoa Makonda taarifa mgonjwa corona

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amekosoa utaratibu uliotumika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutoa taarifa kuhusu kuambukizwa virusi vya corona kwa mtoto wa Mwenyekiti wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, picha mtandao

Amesema kutaja ugonjwa wa mtu ni kwenda kinyume cha taratibu za kitabibu, akiwataka wananchi kuamini taarifa za ugonjwa wa corona zinazotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Waziri wa Afya na Waziri Mkuu.

Sambamba na hilo, amesema hadi sasa Tanzania imejitahidi kudhibiti maambukizo ya ndani kwa ndani ya ugonjwa huo na wasafiri 245 walioingia nchini tangu Machi 23 mwaka huu, wametengwa kwenye hoteli na maeneo yaliyoandaliwa.

Ummy aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari, ambao pamoja na mambo mengine, walihoji uhalali wa taarifa iliyotolewa na Makonda siku tatu zilizopita kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo.

Akijibu swali hilo, waziri huyo alisema kwa mujibu wa taratibu za kitabibu, ugonjwa ni siri kati ya mgonjwa na daktari.

“Suala la RC (Mkuu wa Mkoa) wa Dar es Salaam kwenye hili niseme tu kwa ufupi taratibu za kitabibu zipo wazi, ugonjwa ni siri kati ya mgonjwa na daktari, ndiyo maana kwenye taarifa zangu zote, sijawahi hata siku moja kutaja jina zaidi ya kusema mgonjwa huyu mwanamke au mwanaume na umri wake, na aliingia nchini tarehe fulani.

"Sijataja jina, Isabela alitajwa na baadhi ya watu na yeye mwenyewe alijitaja, na alivyojitaja na sisi tukamtaja, MwanaFA alijitaja mwenyewe, na pia Sallam ambaye ni Meneja wa Mwanamuziki Diamond Platnums," alisema.

Ummy alisema taratibu zinazuia kutaja majina na Rais John Magufuli alishatoa maelekezo kuwa Watanzania waamini taarifa zinazotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya Tanzania na Zanzibar na Waziri Mkuu.

“Sasa kama kuna mtoto wa huyu, ndiyo maana na wenyewe walijitaja, lakini mimi na naibu wangu na Katibu Mkuu hamtatusikia hata siku moja tukitaja jina la mgonjwa kwa sababu ni kinyume cha maadili, miongozo na taratibu za kitabibu nchini," alisema.

Akizungumzia mwenendo wa ugonjwa huo nchini, waziri huyo alisema wizara yake kwa kushirikiana na ya Zanzibar, imeendelea kufanya ukaguzi kwa kupima joto la mwili kwa wasafiri wote wanaoingia nchini.

“Kuanzia Januari Mosi mwaka huu hadi sasa, wasafiri 1,890,532 wamefanyiwa ukaguzi wa kupimwa joto kwenye vituo 27 vya mipakani ikiwamo viwanja vya ndege na bandarini na kwa saa 24 zilizopita, jumla ya wasafiri 3,471 wamefanyiwa ‘screening’,”alisema.

Alibainisha kuwa watu 273 wamepimwa sampuli za kupima virusi vya corona katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii hadi jana huku Zanzibar wakiwa ni 30.

“Kati ya sampuli hizo zilizopimwa, 260 hazikuonyesha uwapo wa virusi hivyo na sampuli 13 zilithibitika kuwa na virusi, wagonjwa hawa ni kutoka Mkoa wa Arusha (2), Dar es Salaam (8), Zanzibar (2) na Kagera (1)," alisema.

Ummy aliongeza kuwa kati ya wagonjwa hao, mmoja ndiyo hakusafiri nje ya nchi katika siku 14 zilizopita kabla ya kuthibitika kuugua na alipata maambukizo kutoka kwa mtu aliyekuwa nje ya nchi.

“Hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa lengo la kutimiza dhamira nzuri ya serikali ya kupunguza hatari ya kusambaa kwa haraka maradhi haya nchini, tunashukuru Mungu bado hatuna 'local transmission' (maambukizo ya ndani kwa ndani),” alisema.

MGONJWA WA KWANZA

Ummy alisema mgonjwa wa kwanza wa Arusha, Isabela, amepona corona na taratibu za kumruhusu kurudi nyumbani zinaendelea, hivyo mkoa huo utabaki na mgonjwa mmoja.

“Mgonjwa wetu amepona COVID19 na amepimwa mara tatu hana, tumeanza utaratibu wa kumrudisha nyumbani, kazi ambayo nimemwelekeza Katibu Mkuu aifanye sasa hivi suala la kutoa elimu ili kuondoa unyanyapaa, kulaumiana na kunyooshewa vidole Isabela,” alisema.

245 WATENGWA

Waziri huyo alisema wasafiri 245 walioingia Tanzania Bara na Zanzibar wamewekwa karantini kwa siku 14 kwenye maeneo maalum yaliyobainishwa na serikali kwa gharama zao.

“Tangu agizo la Rais, wasafiri 111 kwa Tanzania Bara na 134 kwa Zanzibar wametengwa kwenye hayo maeneo, na tunasisitiza mikoa yote nchini kuendelea na zoezi la kubainisha sehemu zitakazotumika kuweka wasafiri bila kuleta usumbufu usio wa lazima,” alisema.

Waziri huyo pia alisema Tanzania imepokea msaada wa vifaa mbalimbali vikiwamo vya kupima virusi haraka (rapid test kits) kutoka kwa taasisi zilizoko Jamhuri ya Watu wa China za Jack Ma na Alibaba na vitasambazwa kwenye hospitali zilizotengwa maalum kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed, aliwataka Watanzania kujikinga na ugonjwa huo huku akisisitiza kuwa serikali haina nia ya kumweka mtu kambini kumtesa.

“Huu ugonjwa tunapaswa kujikinga, mwanangu alishukiwa na akachukuliwa kipimo kuangalia katika kumuuliza akasema amekutana na watu 50 nikiwamo na mimi. Je, tuna uwezo wa kuchunguza watu wote? Mtu atakayepata ishara, ajitokeze na kueleza watu aliokutana nao.

“Hii si kazi ndogo, kila mtu anapiga kelele, sisi Watanzania hali ilivyo tujitahidi kupeana nafasi hii inapunguza maambukizo kwa asilimia 50, tuwasikilize viongozi wetu,” alisihi.

Habari Kubwa