Waziri Jafo: Kanuni Uchaguzi Serikali za Mitaa kufumuliwa

21Jan 2019
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri Jafo: Kanuni Uchaguzi Serikali za Mitaa kufumuliwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema wizara yake inaendelea na mchakato wa kuzifanyia marekebisho kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kukidhi mahitaji ya demokrasia.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo.

Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Jafo, alisema wizara yake inasimamia mchakato wa kuboresha kanuni hizo ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha demokrasia nchini.

“Kwa mwaka huu, wizara yangu ina mambo makubwa. La kwanza ni kuimarisha demokrasia,”

"ofisi yangu ndiyo inahusika katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kwa hivyo, tuko katika mchakato wa maandalizi ya uchaguzi huo.

"Mchakato hivi sasa unaenda vizuri, tumeshaita wadau, hasa katika kanuni zile kuhakikisha uchaguzi unafanyika.

Tayari tumeshaita wakurugenzi wa mamlaka husika za serikali za mitaa ambao watakuwa wasimamizi kule.

"Pia tumeshakutana na ma-RAC, wakuu wa mikoa na wadau mbalimbali tunaendelea kukutana nao kwa lengo la kupata kanuni za kutuwezesha kufanya uchaguzi huo.

“Na kanuni hizi mwaka huu 'tunazi-review' kulinganisha na upungufu uliojitokeza huko nyuma kwa kuyafanyia maboresho zaidi.

"Muhimu kwetu ni kuhakikisha tunasimamia uchaguzi huu vizuri zaidi ili watu waweze kushiriki, kwa sababu serikali za mitaa uchaguzi wake ni muhimu, unagusa kila mahali, hasa kule ambako ndiko wananchi wanachukua viongozi ambao wanapanga nao mipango yao ya maendeleo ya kila siku." 

SIRI YA MAFANIKIO

Mbali na mchakato wa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, Jafo alitaja siri ya kung'ara kwake kiutendaji. Tayari Rais John Magufuli ameshaweka wazi kuwa anakoshwa na utendaji wa waziri huyo.

Waziri huyo alisema kung'ara kwake kiutendaji kunatokana na nidhamu aliyonayo katika kuzingatia muda.

“Hii ndiyo siri yangu ya mafanikio, najali sana muda," Jafo alisema, "maisha yangu yote nimekuwa mtumwa wa muda na nikienda 'site' (eneo la mradi) kama mkoani, maana yake nafanya kazi sana mpaka wakati mwingine watu huwa wananishangaa kwanini nafanya kazi hivyo.

"Mfano juzi juzi nilienda Kibondo, niliongea na watu, nikakagua miradi, nikaenda na Kasuru, nikafanya kazi halafu nikaenda na Kigoma. Hiyo ndiyo 'nature' yangu, na mimi niko makini na suala la muda hasa katika kutekeleza dhamana niliyopewa."

Jafo pia alisema huwa anachukia anapoona watendaji wanashindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao na wizi wa fedha za serikali.

 

BILIONI 105/-

Katika mahojiano hayo, Jafo pia alisema wizaya yake mwaka huu imepanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali za wilaya ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote.

Alisema tayari Rais Magufuli ameshawapatia Sh. bilioni 105 kwa ajili ya hospitali za wilaya 67 na ameshatoa maelekezo kuwa ifikapo Januari 30, awe amepata picha ya ujenzi wa hospitali hizo.

“Kwanza nimshukuru Rais kwa kuniamini na kunipa dhamana katika wizara hii ambayo ni kubwa, nafurahia kwa sababu ‘nature’ yangu pia napenda kufanya kazi kwa bidii na nishukuru kwamba tangu tumepata dhamana hii tumefanya kazi kubwa sana katika sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu, miundombinu, afya na mambo mengine yamefanyika kwa ujumla wake," Jafo alisifu.

“Na sasa ninavyozungumza, tumekamilisha na tunaendelea kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya ambavyo mpaka sasa tunaenda na zoezi la ujenzi wa vituo 350 ambavyo vikikamilika, vitafanya ukombozi mkubwa kwa Mtanzania.”

Alisema wizara yake mwaka huu pia imepanga kutekeleza miradi ya ujenzi na uboreshaji wa barabara.

Alisema wanaendelea kuboresha na barabara zilizoko katika Jiji la Dar es Salaam kupitia mradi wa DMDP na kuboresha barabara zote zilizo katika hali mbaya.

Waziri huyo alisema tayari Sh. bilioni 660 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo na kazi imeshaanza kufanyika.

Alisema kuwa mbali na Dar es Salaam, wanaboresha barabara katika miji mingine saba ikiwamo Arusha, Mbeya, Mwanza, Mikindani na Ilemela ambayo ujenzi unaendelea.

Jafo pia alisema wanaendelea kujenga madampo ya kisasa katika miji ya Dodoma, Arusha, Mikindani, Mwanza na Tanga, akiamini kufikia Desemba mwaka huu, maeneo hayo yatakuwa vizuri.

Alisema kuwa wizara yake mwaka huu imepanga kuboresha miradi ya kuimarisha manispaa na miji, mradi ambao unatarajiwa kugharimu Sh. bilioni 541.

Alisema tayari ujenzi wa barabara za lami unaendelea katika manispaa na halmashauri zote nchini na anaamini mradi huo utakuwa umekamilika kufikia mwakani, huku wakiendelea pia na uboreshaji wa barabara za vijijini.

Jafo alisema mwaka huu wizara yake pia inaendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuboresha zaidi miundombinu.

“Naona sasa hivi watoto wengi wanafaulu na hiyo inaonyesha imani ya wananchi kwa shule za serikali inarudi kama ilivyokuwa zamani," Jafo alisema na kufafanua zaidi:

"Leo hii unaona kwamba matokeo ya kidato cha nne yakitoka, wazazi wengi, hata kama mtoto alikuwa akisoma shule binafsi, wanataka kuwapeleka kidato cha tano katika shule za serikali, na hii inatokana na kasi kubwa ya uboreshaji wa shule zetu."

Alisema serikali inahakikisha shule zinakuwa na vyumba vya madarasa vya kutosha ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu wanaanza masomo kwa wakati.

Alisema tangu serikali ianze kutekeleza ahadi yake ya kutoa elimu bila malipo, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi kujiunga na shule ikiwa ni pamoja na waliokuwa wamekata tamaa ya kusoma.

Jafo alisema wizara yake mwaka huu pia imepanga kuendelea kuwawezesha vijana, kinamama na wenye ulemevu kupata mikopo kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali. Alisema Sh. bilioni 51 zimetengwa kwa ajili ya kuyawezesha makundi hayo.

“Na bahati nzuri tumepitisha sheria kwamba mikopo hiyo itoke kwa utaratibu maalum, tena bila riba.

Eneo hili kwangu mimi ni mtazamo kwamba itasaidia sana hasa katika uanzishwaji wa viwanda vidogo," Jafo alisema.

"Tukumbuke mwaka jana nilitoa agizo kwa wakuu wa mikoa waanzishe viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, kila mkoa uwe na viwanda 100, lengo likiwa ni kupata viwanda 2,600. Faraja niliyonayo ni kwamba kwa ripoti ya awali, viwanda 3,100, kwa hiyo tumepitiliza lengo."

Alisema mwishoni mwa mwezi huu, wanatarajia kutoa ripoti ya tathmini ya viwanda katika mikoa.

Alisema ripoti hiyo itaonyesha nani alifanya vizuri zaidi na kwamba ipo mikoa ambayo imefanya vizuri zaidi kuliko mingine.

Alisema ripoti itaorodhesha mkoa wa kwanza mpaka wa mwisho kwa lengo la kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda nchini.

Katika mahojiano hayo, Jafo alisema kumekuwa na mafanikio na mapinduzi makubwa ya maendeleo katika serikali ya awamu ya tano.

“Miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano ni fahari kubwa kwa Watanzania na maana yake imeweka nyota inayong`ara na watu wengine.”

Habari Kubwa