Zitto amkaribisha rasmi Membe ACT

30Jun 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto amkaribisha rasmi Membe ACT

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amemkaribisha aliyekuwa Kada wa Chama cha Mapinduzi Bernard Membe kujiunga na upinzani ili kuongeza nguvu katika vyama hivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

KIONGOZI MKUU WA CHAMA CHA ACT-WAZALENDO ZITTO KABWE AKIWA NA BENARD MEMBE:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kilwa, Zitto amesema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ana fursa ya kuunganisha Watanzania wenye kiu ya mabadiliko kupitia vyama mbadala vya siasa.

"Ndugu yangu Benard Membe kafukuzwa uanachama wa CCM afanye maamuzi ya kuunganisha nguvu kupitia vyama mbadala ili kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka " Zitto amesema

 

Kiongozi huyo wa ACT ambaye yuko katika ziara ya kichama ya mikutano ya ndani kusini mwa Tanzania, amesema anaelewa mwanasiasa huyo bado anapambana kubaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini muda huu anahitajika zaidi kwenye upinzani.

Katika mahojiano na Kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo kuhusiana na iwapo ana mpango wowote wa kuwania Urais alisema kuwa aumuzi wa kugombea au kutogombea utafahamika pale tu atakapomaliza kuongea na wazee wa mkoa wa Kigoma na kuhusu iwapo chama hicho kimepata ombi lolote kutoka kwa waliokuwa makada wa Chama cha Mapinduzi akiwemo Bernard Membe kujiunga na chama hicho kwa lengo la kuwania Urais alisema hajapata ombi hilo .

Hata hivyo alibainisha kuwa taratibu za chama hicho zipo wazi na kwamba hazimbagui mtu yeyote mwenye nia ya kujiunga na chama hicho kwa lengo la kuwania uongozi. 

Habari Kubwa