Akamatwa na meno mawili ya tembo kwenye banda la mbuzi

04Aug 2021
Neema Hussein
KATAVI
Nipashe
Akamatwa na meno mawili ya tembo kwenye banda la mbuzi

JESHI  la Polisi  mkoani Katavi, linamshikilia Mathias Sikazwe (68) kwa tuhuma za kukutwa na meno mawili ya tembo akiwa ameyahifadhi kwenye banda la kufugia mbuzi.

kamanda wa jeshi la polisi mkoani katavi akionyesa meno mawili ya tembo walioyakamata katika Kijiji cha Igongwe kata Stalike mkoani katavi.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Kamanda wa jeshi hilo, Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo limetokea Agosti 03,2021 katika Kijiji cha Igongwe kata ya Stalike mkoani humo.

Amesema kwa kushilikiana na kikosi cha hifadhi ya Taifa ya Katavi walipata taarifa kutoka kwa raia mwema  na kufanya msako katika nyumba yake na kufanikiwa kumkamata.

"Meno hayo yana uzito wa kg 2.5 ambayo thamani yake bado haijajulikana ila tuna hesabu kwamba alimuua tembo mzima mwenye thamani ya fedha za kimarekani  dola Elfu 20. ", amesema Kuzaga.

Amesema jeshi la polisi bado linaendelea na mahojiano ili kubaini washiriki  wengine waliohusika na tukio hilo pamoja na kubaini siraha iliyotumika kumuua tembo huyo.

Hata hivyo amesema baada  ya upelelezi  kukamilika taratibu zingine za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Kuzaga ametoa wito kwa wananchi wanaojihusha na shughuli  haramu za ujangili kuacha mara moja na badala yake wafanye kazi za halali.

Habari Kubwa