Homera awapiga marufuku walioanza kampeni nyumba kwa nyumba

12Jun 2019
Mary Geofrey
KATAVI
Nipashe
Homera awapiga marufuku walioanza kampeni nyumba kwa nyumba

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, amewapiga marufuku wanasiasa walioanza kujipitisha nyumba kwa nyumba kufanya kampeni kabla ya muda wa uchaguzi uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kufika.

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera.

Homera anatangaza marufuku hiyo, ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu ameteuliwa na Rais John Magufuli  kushika nafasi ya kuuongoza mkoa huo Mei 14, mwaka huu, ambao awali wakuwa unaongozwa na Amos Makalla.

Homera aliyaeleza hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusu maendeleo ya mkoa huo na kusema imeibuka tabia ya wanasiasa kujipitisha kwenye nyumba za watu kuchukua majina ya vitambulisho vya wapiga kura na maelezo mengine.

Amesema muda wa kampeni haujafika hivyo hatawafumbia macho wanasiasa wanalioanza kuvunja sheria za Nec na kusababisha usumbufu kwa wananchi wa mkoa huo.

"Tunatambua kwamba kampeni za kisiasa zina muda wake hivyo ni kosa kwa chama chochote iwe Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha TLP, ACT-Wazalendo au Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kabla ya muda haujafika na atakayekamatwa anafanya hivyo atashughulikiwa," amesema mkuu huyo wa mkoa.

Homera ambaye hakutaja chama kilichoanza kufanya kampeni katika maeneo mbalimbali ya vijiji vya mkoa huo, alisema vyama vyote vinapaswa kusubiri hadi Septemba mwaka huu katika uchaguzi wa Serikali za mtaa ili waanze kampeni zao kwa mujibu wa sheria.

Ameeleza zaidi kuwa, mikutano ya hadhara ya kisiasa ilipigwa marufuku na Msajili wa Vyama vya Siasa na wanaruhusiwa kufanya mikutano ya ndani ambaye hawezi kuizuia.

Amesema kuwapo kwa vuguvugu hilo, kumesababisha usumbufu na hofu kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Mbali na hilo, amesema vitambulisho vya ujasiriamali vinaendelea kutolewa kwa wafanyabishara wote wa mkoa huo na wamefika asilimia 29.

Amesema wakati anakabidhiwa mkoa huo, vitambulisho vya wafanyabiashara viligaiwa kwa wajasiriamali wachache sawa na asilimia tano lakini ndani ya mwezi mmoja wameshagawa asilimia 29.

"Niliingia ofisini Mei 23 mwaka huu na nilikuta ugawaji umefikia asilimia tano lakini hadi sasa tumeshafika asilimia 29 na tunaelekea asilimia 30," amesema Homera.

Amesema wanawatumia watumishi wa umma kugawa vitambulisho hivyo kwa sababu ni rahisi kuwafikia wafanyabiashara wa mkoa huo.

Aidha, amewapiga marufuku watendaji wanaowanyanyasa wafanyabishara wenye vitambulisho katika mkoa huo.

Habari Kubwa