Spika adai halmashauri zina wahasibu wabovu

08Apr 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Spika adai halmashauri zina wahasibu wabovu

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema hoja za ukaguzi zilizobainisha katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), kwenye Halmashauri zinasababishwa kuwepo na wahasibu wabovu.

Akizungumza mara baada ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yusuph Masauni, kujibu swali la Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu, Spika Ndugai alisema katika taarifa ya CAG matatizo yaliyojitokeza yamesababishwa na wahasibu.

“Ukiziangalia unaziona baadhi ya Halmashauri matatizo yaliyojitokeza yamesababishwa na Wahasibu wana uhasibu mbovu wengine wamefanya hivyo halmashauri zingine wakahamishiwa zingine na kila anapohamishiwa anasababisha hati chafu za mashaka eti vocha hazionekani nani anahifadhi kama sio mhasibu,” amesema.

Ameshauri Wizara ya Fedha kuangalia suala la wahasibu wa aina hiyo. Katika swali la Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itatekeleza kikamilifu waraka namba tatu wa Mwaka 2015 kuhusu muundo wa kada ya uhasibu na ukaguzi wa ndani.

“Je, ni lini Kitengo cha uhasibu na fedha katika Wizara na Sekretarieti za Mikoa zitapewa hadhi ya kuwa idara,” amehoji. Akijibu swali la Mbunge huyo, Naibu Waziri Masauni alisema waraka huo ulianza kutekelezwa mnamo mwezi Julai, 2018 kwa kutenganisha kada ya maafisa hesabu na wahasibu.

“Kwa mujibu wa muundo huo mpya Wahasibu ni wale wenye CPA na wale wasio na CPA wanatambulika kama Maafisa Hesabu,”amesema.

Aidha, amesema kuhusu kupandisha hadhi vitengo vya uhasibu na fedha katika Wizara na Sekretarieti za Mikoa kuwa idara, katika kuandaa miundo ya taasisi, vigezo kadhaa hutumika ili kufikia maamuzi ya kuwa idara, vitengo na sehemu.

“Kwa kuwa miundo hii hufanyiwa marekebisho mara kwa mara kwa kushirikiana na wataalamu wa miundo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma (OR-MUU) na kujadiliwa katika ngazi ya maamuzi (PIC), ni mategemeo yetu kwamba serikali itakapoona kuwa kitengo cha uhasibu na fedha kinakidhi vigezo kuwa idara, kitapewa hadhi hiyo,”amesema.

Habari Kubwa