Watumiaji mitandao ya kijamii waonywa

14Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
  Watumiaji mitandao ya kijamii waonywa

WATUMIAJI wa mitandao na jamii wametakiwa kuacha kutangaza na kuweka hadharani picha ama kutaja majina ya watoto wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai kwa kuwa ni kinyume cha Sheria mpya ya mtoto ya mwaka 2009.

Rai hiyo imetolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Ziwa, Robert Makaranga, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utekelezaji wa sheria hiyo namba 21, wafanyakazi na wadau wanaohusika na kutetea haki mbalimbali za watoto kufuatia kuanzishwa kwa mahakama mbili za watoto nchini katika mikoa ya Mbeya na Dar es Salaam.

“Tumeona baadhi ya watumiaji wa mitandao na wananchi wachache  wana tabia ya kutangaza majina ya watoto wanaotuhumiwa katika makosa ya jinai pamoja na kupiga picha zao na kuzionyesha mitandaoni, sasa naomba ieleweke kufanya hivyo ni marufuku chini ya sheria hii,  ukitofautisha na zile sheria za mitandaoni kwa sababu mtoto akivunja  sheria hawezi kukuzeeka na lile kosa,” alisema Jaji Makaranga.

Hata hivyo, alisema kwa sasa serikali haina gereza la watoto, isipokuwa kuna shule moja maalumu ya kurekebisha tabia za watoto wanaovunja sheria ambayo ipo mkoani Mbeya, iliyoanzishwa kwa lengo la kufundisha watoto kuishi vyema mbele ya jamii inayowazunguka na baadae wanakuwa watu wazima.

 

Habari Kubwa