CCM yashinda Ushetu

10Oct 2021
Shaban Njia
Nipashe Jumapili
 CCM yashinda Ushetu

MSIMAMIZI wa uchaguzi Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga, Mwalimu Lino Mwageni amemtanga mgombe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Emmanuel Cherehani kuwa mbunge mteule wa jimbo hilo baada ya kupata kura 103,357 sawa na asilimia 96.6 ya kura zote zilizopigwa jimboni hapo.

Awali vyama vya siasa 16 vilijitokeza kuchukua fomu ya kugombea jimbo hilo lakini vyama 14 vilikosa sifa na baadhi yao kushindwa kurejesha fomu mpaka muda ulipokwisha huku chama cha CCM na ACT Wazalendo vikikidhi vigezo na kugombea.

 

Akitangaza mataokea hayo majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo, Mwageni alisema kuwa,idadi ya wapiga kura walikuwa 165,418 lakini waliopiga kura walikuwa  107,188 katika vituo vyote 457 vilivyokuwa vimeandaliwa katika jimbo zima. 

Aidha alisema kuwa,kati ya kura hizo idadi halali ya kura zilizopigwa zilikuwa 106,945, idadi ya kura zilizokataliwa zilikuwa kura 243, huku mgombea wa chama cha ACT Wazalendo, Julius Mabula akipata kura 3,588 sawa na asilimia 3.4. 

Hata hivyo Mwageni, alisema kuwa mpaka anatangaza matokea hayo hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza katika vituo vya kupiga kura, hivyo uchaguzi ulikuwa wa huru na haki na wananchi walijitokeza vile ilivyowezekana. 

Uchaguzi  mdogo wa jimbo hilo umefanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Elias Kwandikwa kufariki dunia Agosti 2 mwaka huu. 

Habari Kubwa