​​​​​​​Mbinu tisa za shule binafsi kushikilia watoto saa nyingi

05Dec 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
​​​​​​​Mbinu tisa za shule binafsi kushikilia watoto saa nyingi

​​​​​​​BAADA ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu kupiga marufuku wanafunzi kusoma saa za ziada siku na wakati wa likizo shuleni, Nipashe imebaini mbinu tisa zinazotumiwa na shule binafsi kufanikisha upotoshaji huo.

Ni marufuku aliyoitangaza waziri Jumanne wiki hii, akizingatia taarifa za athari kwa wanafunzi zilizotolewa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) siku chache kabla, kikitangaza kuanza utafiti wa kiafya kwa watoto wanaokaa muda mrefu masomoni, pia kulazimishwa kubeba mizigo mizito ya vitabu.

 

Nipashe ambayo imekuwa ikifuatilia suala hilo kwa mwaka huu wote, imebaini namna shule binafsi zinavyowahadaa wazazi na uongozi wa kiserikali kusifahamike madhila hayo kwa watoto, lengo ni kufanikisha soko kupitia ufaulu, pia mapato zaidi kupitia ada.

 

Mbinu hizo zilizothibitishwa hata na baadhi ya walezi, zinajumuisha kuwahadaa kwenye mikutano ya wazazi; kuwahamishia wanafunzi bwenini; ada kubwa kulipwa mwanzoni mwa mwaka; wanafunzi huhamia bwenini baada ya agizo la ada kutimizwa; kuwamiliki waratibu elimu kata na mtoto kudhibitiwa kutoa siri za bweni.

 

Zingine zinajumuisha; kutumia umaarufu wa shule kama hoja ya 'kuwateka' wazazi; Jumamosi na Jumapili wanafunzi hawavai sare ilhali wanaendelea na ratiba ya masomo kama siku zote na inapotokea mkasa, kinga yao kuu jumuiya za umoja wao kuja na utetezi wa pamoja.

 

Nipashe ilibaini shule ambazo wanafunzi wanakuwa masomoni kwa kati ya saa 12 hadi 14 kwa siku sita za wiki, huku baadhi yao zikiwamo za wilayani Ilala, zinaendesha ratiba hizo kwa siku zote za wiki.

 

Nipashe ilithibitishiwa na mzazi Simon (jina la pili tunalo) sambamba na mtumishi wa shule mojawapo (jina tunalo), akieleza hatua ya kwanza ni kwamba hoja huibuliwa kwenye mkutano wa wazazi shuleni kuhusu haja ya saa za ziada kwa watarajiwa wa mitihani ya taifa, ikiendana na darasa hilo lote lihamie bwenini.

 

Imegundulika baada ya ajenda hiyo kupita, mzazi Simon aliyejitambulisha kwa sura ya pili kwamba ni mwathirika wa mtoto wake, aliithibitishia Nipashe hatua inayofuata baada ya mkutano kuwa ni kuwatangazia rasmi wazazi nyongeza ya ada, sehemu kubwa (wastani asilimia 60) kulipwa mara moja baada ya watoto kuingia bwenini.

 

Kwa mujibu wa mzazi huyo, hoja ambayo gazeti hili iliibaini katika shule kadhaa, ni kwamba wakati wote mbinu kubwa ya kujinadi inayotumiwa na shule zinazofanya vizuri ni kuwa hiyo “ndiyo silaha ya ufanisi na ushindi”.

 

Inaelezwa kuwa pindi tu wanafunzi wanapoingia katika maisha hayo mapya ya bwenini ndio unakuwa mwanzo wa madhila dhidi yao kwa madai wako hapo kwa baraka za wazazi, ikiendana na amri kali ya wasitoe siri ya maisha yao bwenini, pia ratiba za kuonana na wazazi hudhibitiwa.

 

Lingine lililogunduliwa kwenye uchunguzi huo, uongozi wa shule hujenga uhusiano wa karibu na ofisi ya mratibu elimu wa eneo lao ili kupata utetezi, jambo ambalo mzazi Simon alikiri kulishuhudia, hata kumpa mazingira ya kiulizo kwenye mkasa uliohusu msuguano wake na shule kuhusu alichokiita uonevu kwa mwanawe katika shule ya jijini Dar es Salaam.

 

Mbinu nyingine iliyobainika ni kwamba ili kuficha siri na ratiba ya maisha ya wanafunzi walio bwenini na hata wachache kuwa nje ya bweni, kwa siku za wikiendi (Jumamosi na Jumapili) hawavai sare, ila ratiba zao za masomo zinabaki vilevile.

 

Nipashe katika uchunguzi wake ililazimika kuuhoji uongozi wa mamlaka husika inayosimamia shule binafsi nchini mapema mwaka huu na iliitolea ufafanuzi unaokinzana na maelekezo ya sera ya elimu inayotumika nchini.

 

SERA ELIMU INASEMAJE?

 

Sera ya Elimu ya Msingi Toleo la Tatu la Mwaka 2019 inaelekeza mwanafunzi akae darasani kwa siku tano za wiki, ikiwa na jumla ya muda usiozidi saa 30, ikifafanua: “Mwaka wa masomo utakuwa na siku 194 ambazo ni sawa na wiki 39 kwa  Darasa la III–VI.

 

"Darasa la VII watakuwa na wiki 34 kutokana na darasa hilo kuwa na mtihani wa mwisho mwezi Septemba kila mwaka.

 

“Mwaka umegawanywa katika mihula miwili ya masomo. Kila muhula utakuwa na wiki mbili zitakazotumika kwa mitihani. Muda wa kusoma utakuwa ni saa sita kwa siku kwa Darasa la III–VII. Muda wa kipindi ni dakika 40. Kutakuwa na vipindi vinane kwa siku kwa wanafunzi wote isipokuwa siku ya Ijumaa ambayo itakuwa na vipindi sita.”

 

Kwa mujibu wa sera hiyo, wanafunzi watasoma vipindi 38 kwa wiki, ambayo ni sawa na jumla dakika 1,520 ambayo ni sawa na saa 25 na dakika 33; hiyo inaangukia wastani wa saa tano kwa kila siku ya masomo, uwiano unaoonyesha wastani wa saa sita uliotajwa kwenye sera, unajumuisha muda wa ziada wa mengineyo kama mapumziko.

 

USHUHUDA WA MWANAFUNZI

 

Mwanafunzi (jina tunalo) mhitimu wa darasa la saba, kutoka shule ya mkoani Dar es Salaam, aliiambia Nipashe kuwa wote walio darasa la saba waliishi bwenini kwa ratiba ya saa 14 masomoni kati ya saa 12 asubuhi na saa nne usiku kwa siku za Jumatatu hadi Jumamosi.

 

Kwenye ratiba hiyo yenye ziada ya saa nane kila siku masomoni ikiwamo Jumamosi ikilinganishwa na maelekezo ya sera, alisema Jumapili ratiba yao ilianzia kwenye ibada saa tatu asubuhi na baada kula mchana, waliingia masomoni ratiba ikiisha kati ya saa mbili na saa nne usiku.

 

Akianisha mpangilio wa ratiba hiyo kila siku iliyowashurutishwa mara nyingi kufua nguo zao usiku baada ya kutoka darasani, waliamshwa saa 10 alfajiri kujiandaa kisha kupelekwa na gari la shule hadi wanakosoma kutoka mbali wanakolala, lakini dada zao waliishi jirani na madarasa.

 

Huku akikumbuka maisha ya uchovu alioupata, alisema masomo yalianza rasmi saa 12 asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa cha uji, kisha kifungua kinywa kingine katika mapumziko ya nusu saa nne asubuhi, kisha mchana saa saba walipumzika kwa saa moja ya mlo ya kurudi darasani.

 

Alisimulia kuwa saa 11 jioni walipumzika nusu saa wakinywa uji na kurudi darasani hadi saa mbili usiku na baada ya nusu saa walirudi tena darasani hadi saa nne usiku kukamilisha ratiba ambayo hata wenzao wachache walioishi nyumbani kutokana na hitilafu za kiafya, wazazi wao walilazimika kuwafuata.

 

USHUHUDA WA MZAZI

 

Mzazi Simon anasimulia namna alivyogundua kuwapo jambo nyuma ya pazia kupitia kikao cha wazazi shuleni, pale alipoanza kulazimishwa mtoto wake mwenye hitilafu kiafya akae bwenini, pia kushindwa kupewa uthibitisho wa kisheria unaoendana na ratiba hiyo yenye ziada nyingi hasi ambazo hazikuanishwa kwenye mkutano wa wazazi. Alikuwa tayari alishalipa ada.

 

Aliieleza Nipashe kushangazwa na Mratibu wa Elimu wa eneo hilo (jina tunalo) namna ushirikiano na uamuzi wa jambo hilo ilivyoelemea upande mmoja, huku akitetea ratiba hiyo ni uamuzi wa wazazi shuleni, naye anauheshimu.

 

Simon alisema hata pale alipohoji nafasi ya Sera ya Elimu ambayo ndio mwongozo mkuu katika kufafanua jambo hilo kwenye kikao cha pamoja, bado mratibu huyo hakutoa ushirikiano wa ufafanuzi wake huku mamlaka ya shule ikitamtakia ”hiyo sera ni kwa ajili ya shule za serikali.”

 

Kwa mujibu wa mzazi huyo, awali uongozi wa shule haukuwa tayari kumrejeshea ada ya mwanawe aliyekuwa na shida kiafya, lakini alishangaa miezi kadhaa baadaye aliombwa kama anaweza amhamishe mtoto pasipo ada kurejeshwa, jambo alilolikataa na kuliwasilisha kisheria katika ngazi ya halmashauri walikotatua mara moja baada ya Mratibu Elimu kushindwa.

 

Awali Nipashe ikifuatilia suala hilo lililoonekana kumea kwenye shule kadhaa za Dar es Salaam na kumdadisi Katibu Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyokuwa vya kiserikali (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya, aliyekiri kuwapo ratiba ya ziada shuleni akitaja sababu kubwa ni kufidia muda wa ziada kutokana na shule kufungwa miezi kadhaa dhidi ya corona.

Habari Kubwa