​​​​​​​Serikali kukabidhi MV Butiama, Victoria na Chelezo muda wowote

26May 2020
Dotto Lameck
Mwanza
Nipashe
​​​​​​​Serikali kukabidhi MV Butiama, Victoria na Chelezo muda wowote

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, amesema serikali itakabidhi meli ya MV Butiama, MV Victotia na Chelezo wakati wowote kuanzia sasa baada ya ukarabati mkubwa uliofanyika kukamilika kwa asilimia 99.

Mafundi wa Kampuni ya Kampuni ya Songoro Marine Limited, wakikamilisha kazi ya upakaji rangi kwenye meli ya MV. Butiama.

Nditiye amesema hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli ya MV Mwanza huku akisema kuwa kutokana na kufunguliwa kwa anga la Tanzania kutaruhusu wataalamu kutoka nje kuja kukamilisha kile kilichobaki.

“Tungekuwa tushaanza kuzitumia meli hizi kwani ukarabati wake umekamilika kwa asilimia 99, ni imani yangu kuwa wataalam wanaosubiriwa watawasili siku chache zijazo na kukamilisha kile kilichobaki ili wananchi waanze kutumia usafiri huu’ amesema Mhandisi Nditiye.

Muonekano wa Chelezo (kulia) ambacho tayari kimekamilika.

Aidha, amesema pamoja na miradi hiyo mradi wa meli mpya ya MV Mwanza ujenzi wake unaendelea kwa kasi na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2021.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Eric Hamis, ameishukuru serikali kwa kukamilisha malipo yote ya mradi wa ukarabati wa meli hizo pamoja na chelezo na kuahidi kuendelea kuisimamia kwa karibu ujenzi wa meli mpya unaoendelea.

Naye Meneja Mradi wa Meli mpya ya MV Mwanza, Mhandisi Vitus Mapunda, amesema mradi wa meli hiyo unaendelea vizuri na kazi zinazoendelea kwa sasa ni kukamilisha tabaka la chini la meli hiyo kabla ya kuiweka kwenye chelezo.

Mafundi wa Kampuni ya Gas Entec kutoka Korea ya Kusini, wakiendelea na kazi ya ujenzi wa meli Mpya ya MV Mwanza katika bandari ya Mwanza South.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhandisi Nditiye amekagua maendeleo ya ukarabati wa jengo la abiria katika bandari ya Mwanza North na kutoa wiki moja na nusu ukarabati huo kukamilika.

Hata hivyo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mwanza, Michael Palangyo, amemthibitishia Naibu Waziri Mhandisi Nditiye kuwa mradi huo wa ukarabati utakamilika kwa wakati na kwa kiwango kikubwa ili kuweza kutoa huduma bora wakati meli za MV Butiama na Mv Viktoria zitakapoanza kutoa huduma kwa wakati wa Mwanza, mikoa ya jirani na visiwa vinavyozunguka mkoa huo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto), akimsikiliza Meneja Mradi wa meli mpya ya MV Mwanza, Mhandisi Vitus Mapunda, wakati akimweleza namna ya ukataji wa vyuma.

Habari Kubwa