‘Elimu ya VVU, TB inahitajika migodini'

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
KAHAMA
Nipashe
‘Elimu ya VVU, TB inahitajika migodini'

MKURUGENZI wa Shirika lisilo la Kiserikali la SHDEPH+, Venance Mzuka, amewashauri wachimbaji wadogo wa dhahabu wilayani Kahama mkoani Shinyanga kujenga utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara,-

hasa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kuwa mazingira yao ya kazi ni rahisi kwao kuambukizwa.

Mzuka alitoa rai hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, akieleza kuwa elimu ya dalili za TB na maambukizo ya VVU inahitajika kwa wachimbaji wadogo ili watambue namna ya kujikinga.

Alidai wachimbaji hao ni rahisi kupata ugonjwa wa TB na maambukizo ya VVU kutokana na mazingira wanayoyafanyia kazi kuwa na mwingiliano wa watu wengi.

Alisema TB huambukizwa kwa njia ya hewa, hivyo ni rahisi kwa makundi yenye mwingiliano mkubwa wa watu kupata ugonjwa huo bila yenyewe kujitambua.

"Wachimbaji wadogo wanafanya kazi zao katika mazingira ambayo si salama, hawana vifaa vya kazi, wanapolipua miamba na usagaji wa mawe ya dhahabu, hutokea vumbi kubwa ambalo huingia kwenye miili yao na kuathiri mapafu na kusababisha wao kuwa na urahisi wa kupata TB," Mzuka alisema.

Meneja Mradi wa TB, Ereneus Nwinuka, alisema ugonjwa huo bado ni changamoto nchini na ndiyo sababu ya kuamua kuweka maofisa katika kila kata ya Halmashauri za Mji wa Kahama na Msalala.

Alisema maofisa wao hao hupita nyumba kwa nyumba kutoa elimu kuhusu chanzo, dalili na madhara ya TB.

Kuhusu VVU, meneja huyo alisema watu wanaoishi na VVU mara nyingi hupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa TB kwa kuwa vimelea vya ugonjwa huo hushambulia mapafu na kusababisha kushindwa kufanya kazi yake vizuri.

Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, Shea Nassoro, alibainisha kuwa mwitikio wa upimaji wa TB ni mdogo katika jamii ukilinganisha na mwitikio wa upimaji wa maambukizo ya VVU kutokana na suala hilo kutopewa uzito.

Nassoro aliwashauri wachimbaji wadogo na watu wanaoishi pembezoni mwa migodi, kujenga utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya magonjwa nyemelezi ikiwa ni pamoja na TB na maambukizo ya VVU.

 

 

Habari Kubwa