‘Malkia wa Tembo’ ahukumiwa upya

08Dec 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
‘Malkia wa Tembo’ ahukumiwa upya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu upya kifungo cha miaka 9 jela malkia wa meno ya tembo, Yang Feng Glan na wenzake wawili baada ya kuwatia hatiani kwa makosa matatu ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh. bilioni 13.9.

Washtakiwa hao walihukumiwa kwa mara ya kwanza na kupewa adhabu ya miaka 15 jela kuanzia Februari mwaka 2019, Mahakama Kuu ilifuta adhabu na kuamuru jalada kurudi Mahakama ya Kisutu kwa kuandika hukumu upya ambapo jana walisomewa hukumu yao.

Mbali na Malkia wa meno ya tembo, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Salvius Matembo na Philemon Manase.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema hukumu dhidi ya washtakiwa hao ilishatoa mwaka 2019, walikata rufani Mahakama Kuu ambapo katika uamuzi wake iliamuru jalada lirejee Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Alisema Mahakama Kuu ilielekeza hukumu iandikwe upya na ielezwe washtakiwa walitiwa hatiani kwa makosa gani.

"Washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu, kujihusisha na mtandao wa uhalifu makosa mawili na kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo.

"Hoja iliyopo kuangalia je, washtakiwa wanajuana? Kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri imethibitika kwamba washtakiwa wanajuana.

"Mashahidi walielezea mshtakiwa wa kwanza na wapili walivyofahamiana katika biashara ya meno ya tembo, ilionyesha walikuwa wanakusanya na kupeleka kwa malkia.

"Mshtakiwa watatu, Malkia ushahidi ulionyesha alipokea, alipima na kuficha na kati ya mshtakiwa wa kwanza na wapili kulikuwa na miamala ya kutumiana fedha, walishindwa kueleza fedha hizo zilikuwa za nini," alisema Hakimu Shaidi.

Alisema kuhusu kufahamiana, ushahidi umebainisha kuwa walikuwa wanafahamiana washtakiwa wote watatu.

"Mahakama imejiridhisha kwamba makosa yalithibitika bila kuacha shaka yoyote, Mahakama inamtia hatiani mshtakiwa wa tatu Malkia kwa kosa la kujihusisha na genge la uhalifu, inawatia hatiani mshtakiwa wa kwanza na wapili kwa kosa la kujihusisha na genge la uhalifu na inawatia hatiani washtakiwa wote kwa kosa la kujihusisha na biashara ya meno ya tembo," alisema.

Baada ya washtakiwa kutiwa hatiani, Wakili Nehemiah Nkoko aliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa kuzingatia tayari walishatiwa hatiani, walianza kutumikia kifungo kabla ya Mahakama Kuu kufuta adhabu hiyo.

Alidai Mahakama Kuu ilisema washtakiwa walikaa gerezani miaka sita, lakini kwa kuangalia mwaka wakioshtakiwa 2014, walikaa miaka zaidi ya saba.

Wakili Nehemiah alidai Malkia kwa sasa ana miaka 70 na mgonjwa, hivyo aliomba apunguziwe adhabu kutokana na umri wake mkubwa.

Wakili wa Serikali, Faraja Nguka, aliomba pamoja na kupewa adhabu inayostahili, shamba la Malkia lililopo Muheza Tanga litaifishwe na kuwa mali ya serikali.

Akitoa adhabu Hakimu Shaidi alisema alizingatia hoja za pande zote mbili, ni kweli walikaa gerezani muda mrefu, walianza kutumikia kifungo kabla Mahakama Kuu haijatoa hukumu.

"Mliwakosea Watanzania wote, mliua au kusababisha tembo wengi kuuawa, tembo ni chanzo cha mapato ya fedha za kigeni, mshtakiwa wa kwanza na wapili ni Watanzania, lakini mliamua kujinufaisha wenyewe.

"Mshtakiwa watatu, wewe ni raia wa kigeni ulikaribishwa na uliamua kufanya ulichofanya kana kwamba nchi ilikosea kukukaribisha, chezeni mziki wenu, mlioupiga wenyewe," alisema Hakimu Shaidi.

Baada ya kusema hayo alitoa adhabu, kwa kosa la kwanza la kujihusisha na genge la uhalifu Malkia atakwenda jela miaka 15, kosa la pili kama hilo, washtakiwa wawili waliobakia watakwenda jela miaka 15.

Katika kosa la tatu washtakiwa wote watalipa faini mara mbili ya thamani ya meno ya tembo Sh. bilioni 13.9 ambayo ni sawa na Sh. bilioni 27.8, endapo watashindwa watakwenda jela miaka miwili na adhabu zinakwenda kwa pamoja.

Alisema Mahakama inatoa amri ya kulitaifisha shamba la malkia lililoko Muheza Tanga kuwa mali ya serikali.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari mosi na Mei 22, mwaka 2000, maeneo mbalimbali nchini.

Wanadaiwa kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo 860 ambayo ni sawa na tembo 430 yenye kilo 15,900 bila kuwa na kibali.

Mahakama imepunguza miaka sita kutoka 15 ambayo hakimu huyo, aliwahukumu jana kabla ya kupunguza, hivyo kuwa miaka tisa imezingatia ukweli kwamba walikaa muda mrefu gerezani miaka sita.

Habari Kubwa