‘Marufuku ujenzi bila kibali’

13Jan 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
‘Marufuku ujenzi bila kibali’

SERIKALI imepiga marufuku shughuli zozote za ujenzi kufanyika maeneo ya mijini bila kuwa na kibali, huku kukiwa na tishio la kubomoa nyumba zilizojengwa pasipo vibali vya mamlaka husika.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, picha mtandao

Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa mtaa wa Ndachi Kata ya Mnadani katika ziara yake ya kutembelea eneo hilo na eneo la Nkuhungu Broad Acer, jijini Dodoma.

Akikagua nyumba zilizojengwa kwenye eneo hilo bila vibali, alisema jambo hilo halitakubalika na sheria inaruhusu kubomoa nyumba za aina hiyo.

Aidha, waziri huyo aliweka alama ya X kwenye nyumba ambazo wamiliki wa viwanja wameanza ujenzi bila kuwa na vibali kutoka Ofisi ya Ardhi ya jiji hilo, na kuamuru kusitisha ujenzi huo.

Akiwa katika eneo hilo alimpigia mmoja wa wamiliki ambaye ni mtumishi wa umma ambaye mafundi walikutwa wakiendelea na ujenzi bila vibali.

“Ninataka nione hati yako, kibali cha ujenzi, unajua mtumishi wa umma hujengi mahali hadi uwe umemiliki na kupewa kibali cha ujenzi na Manispaa, kwanini umeamrisha pajengwe,” alihoji.

“Samahani waliniambia huku hawana vibali kwa kuwa ni pembezoni mwa mji,” alijibu dada huyo na waziri kusema: “Sheria haijasema pembezoni mwa mji watu wajenge tu, sasa usiendelee kujenga nasimamisha leo, mwambie fundi wako aache kujenga na ujenzi hadi upate kibali.”

Akizungumza na wananchi hao, alisema: “Mtu yeyote anayejenga mjini mahali popote bila kufuata utaratibu wa kumilikishwa yaani kiwanja ambacho hakijapimwa, hujamilikishwa, huna kibali cha wenye mamlaka ya mji unaohusika ujue unajipeleka kwenye hatari ya kuvunjiwa na kuondolewa jengo lako.”

“Msinijaribu na msimjaribu Mahenge (Mkuu wa Mkoa wa Dodoma), sisi serikali tuna nguvu, ole wenu tukute vyoo vinajengwa, mapagale yanajengwa tutayavunja, tumeshavumilia vya kutosha,” alisema.

Kwa mujibu wa Lukuvi, kila anayejenga hata kama ana pagale au msingi serikali itatafuta namna ya kumilikisha, na kwamba kwa sasa wanatakiwa kuacha wapime zipatikane barabara, viwanja vya watoto na ndipo umilikishaji uendane na ukubwa wa viwanja, na ujenzi waanze baada ya kupata vibali.

“Urasimishaji unaofanyika sasa ni huruma ya Rais, lakini kwa sheria ilitakiwa ni marufuku kuwabariki watu waliojenga kwa kuvunja sheria bila vibali, Rais aliniagiza waliotoa jasho lao wakajenga mjini wasivunjiwe ndiyo maana tunarasimisha makazi,” alisema.

Aidha, Waziri Lukuvi alisema serikali haina mpango wa kubomoa nyumba za wananchi isipokuwa wanatakiwa kujenga kwa kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha ujenzi.

Wakati huo huo, Waziri Lukuvi amefanikiwa kutatua mgogoro wa ardhi kwa wakazi wa Ndachi jijini Dodoma uliodumu kwa takribani miaka 14.

Aidha, ametoa miezi mitatu kwa Halmashauri ya Jiji, Idara ya Ardhi Mipango Miji na Rasilimali Watu kuhakikisha wanakamilisha upimaji na urasimishaji katika eneo hilo.

Alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na kwamba serikali imeamua kuumaliza kwa kurasimisha wananchi waliojenga kiholela na kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa.

Aidha, Waziri Lukuvi baada ya kusikiliza wananchi na kupitia hati zao ilibainika kuwa asilimia kubwa ya hati zimemaliza muda wake wa miaka 33 tangu zitolewe mwaka 1985, na kusisitiza kuwa kwa sasa ardhi hiyo siyo mali yao bali ni mali ya Rais hivyo irejeshwa kwake kwa matumizi yanayotolewa mwongozo upya.

ONYO KWA WANANCHI WAKOROFI

Aliwaonya wananchi wa eneo hilo wenye tabia ya kutumia silaha kama mapanga na mishale na kuzuia watumishi wa serikali kufanya kazi yao kuacha tabia hiyo mara moja.

"Ninyi mnaojifanya mnajua kutumia silaha za upinde, mishale, sime na mapanga, muache tabia hiyo mara moja, maana serikali ina silaha za moto… sasa ole wenu muwazuie watendaji wa Jiji kufanya kazi yao ya upimaji na kuchelewesha kazi hiyo, tutawashughulikia ba’rabara," alisema Lukuvi.

Alisema baada ya wananchi hao kupimiwa, watalipa gharama za kodi ya serikali zitakazokuwa zimepangwa na kuruhusiwa kuanza ujenzi au kuendelea na ujenzi.

Habari Kubwa