‘Mchakato wa M/kiti CCM, kutumika mgombea urais Z’bar 2020’

16Jan 2017
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
‘Mchakato wa M/kiti CCM, kutumika mgombea urais Z’bar 2020’

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema wembe uliotumika kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mchakato wa Chama cha Mapinduzi, ndiyo utakaotumika kumpata mgombea wa urais mwaka 2020.

Balozi Seif Ali Iddi.

Alisema wembe huo ndiyo silaha pekee itayosaidia kusafisha virusi na wagombea wa makundi ambao wanaweza kuleta madhara na kuzorotesha umoja na mshikamano kwa wanachama wake kama ilivyotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais mwaka 2015.

Tamko hilo amelitoa nyumbani kwake Kama, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, wakati akizungumza na viongozi wa CCM, Kata ya Mtoni, Jimbo la Temeke, Mjini Dar es Salaam, waliopo Zanzibar kwa mwaliko wa wenyeji wao Kamati ya Ujirani Mwema ya Mkoa wa Magharibi Unguja.

Alisema Chama cha Mapinduzi, hakitawaonea haya wanachama wowote wenye sura mbili na itakapobidi italazimika chama hicho kusafisha taka taka hizo hasa katika kipindi cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi ndani ya chama chenyewe.

Makundi ya wagombea wa urais yameibuka mapema Zanzibar na kuwagawa wanachama na viongozi wa serikali kutokana na joto la kisiasa linaloendelea kupanda tangu kuibuka kwa mgogoro wa uchaguzi mkuu.

Aidha, Balozi Seif alisema inasikitisha kuona wapo viongozi wa chama hicho waliowahi kudiriki kununua kadi cha chama na kuwapa baadhi ya watu wakiwamo wapinzani ili wawachague katika kura za maoni na hatimae wapinzani hao walitumia mwanya huo kuvuruga malengo na mikakati ya chama hicho.

Aliwakumbusha viongozi na wanachama wa CCM walazimike kufanya kazi ya ziada katika kuwabaini wanafiki hao wenye sura mbili wanazozitumia kutoa maamuzi yao wakati wa uchaguzi ndani ya chama.

Akizungumzia maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif alisisitiza masuala hayo yataendelea kuwa na umuhimu kwa Wazanzibari na Watanzania wote katika kujikumbusha mzizi wa fitina wa kikolini uliokatwa na waasisi wa Mapinduzi hayo mwaka 1964.

Balozi Seif alisema zaidi ya miaka 200 iliyopita kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, wakwezi na wakulima wa Visiwa vya Zanzibar, walikuwa wakinyanyaswa kimaisha, madhila yaliyoamsha ari kwa waasisi wa ASP kuandaa mipango ya kujikomboa kwa hali yoyote ile.

Aliwahakikishia viongozi na wanacham wa CCM kwamba yale yote yaliyoasisiwa na viongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kuhusiana na masuala ya elimu, afya na eka tatu tatu walizopewa wananchi bila ya malipo kuendesha maisha yao, yataendelea kutekelezwa daima.

Aliwapongeza viongozi na wananchama wa CCM, Kata ya Mtoni na wenyeji wao Kamati ya Ujirani mwema ya Mkoa wa Magharibi kwa uamuzi wao wa kuanzisha safari za ujirani mwema, unaowapa fursa za kutembeleana kila mwaka.

Alisema utaratibu waliouanzisha ni vyemna wakaendelea kuudumisha kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT ), Kata ya Mtoni, Jimbo la Temeke ambae ndiye kiongozi wa msafara huo, Khadija Said Mkwere, alisema ziara ya ujumbe wake imetoa nafasi kubwa kujifunza mambo mbali ya historia ya Zanzibar na ya Chama cha Mapinduzi.

Mkwere alisema wao kama viongozi wa chama, wataendelea kulinda na kudumisha misingi ya Mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao umesadia kuimarisha umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.

Habari Kubwa