‘Rais wa Tanga’ jela miaka 30 kusafirisha dawa za kulevya

21Nov 2020
Boniface Gideon
Tanga
Nipashe
‘Rais wa Tanga’ jela miaka 30 kusafirisha dawa za kulevya

JANA Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu Kama Mahakama ya Mafisadi, imemhukumu mfanyabiashara Yanga Omary  maarufu  kama  'Rais wa Tanga', kifungo cha miaka 30 baada ya kumkuta na hatia ya kusafirisha gramu 1052.63  ya dawa za kulevya aina ya Heroine.

Mkurugenzi  Msaidizi wa Ofisi ya Mashtaka nchini, Faraji Nchimbi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga jana, baada ya Mahakama ya Uhujumu Uchumi Tanga, kumhukumu mfanyabiashara wa mkoani humo, Yanga Omary maarufu kama Rais wa Tanga, kwenda jela miaka 30 kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. PICHA: BONIFACE GIDEON

Hukumu hiyo  iliyohudhuriwa na  wakazi wengi  wa  Mkoa  wa Tanga imetolewa na Jaji  Immakulata Banzi leo jijini hapa.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji  Immakulata  Banzi alisema  ametoa adhabu hiyo baada kusikiliza maelezo ya pande zote na kumkuta na hatia ya kujihusisha na dawa za kulevya.

Pamoja na hukumu hiyo Jaji banzi alisema mali za Omary likiwamo gari aina ya Toyota Landcruiser, ambalo alikutwa nalo akiwa amehifadhi dawa, hazitataifishwa  kwa kuwa sio mali zake.

Hata hivyo, mahakama hiyo iliwaachia huru  mke wa mfanyabiashara huyo,  Rehema Ally,  na mfanyakazi wa ndani,  Halima Mohamed,  baada ya kukosekana ushahidi  kuwa walijihusisha  na biashara hiyo.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Agosti na Oktoba, 2018  mshtakiwa huyo na wenzake wawili walikamatwa mtaa wa Bombo jijini Tanga wakitaka kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Akizungumza nje ya Mahakama, Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka, Faraja Nchimbi, alisema hukumu ni mwendelezo wa kesi za watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.

Aliwataka  watu wanaojihusisha  na biashara hiyo kuacha mara moja kwa kuwa  serikali itawashughulikia  wote pamoja na kuvunja mitandao  ya watu hao.

Habari Kubwa