‘Saratani yoyote kwa watoto inatibika’

02Sep 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
‘Saratani yoyote kwa watoto inatibika’

IMEELEZWA kuwa ugonjwa wa saratani yoyote kwa watoto unatibika kwa zaidi ya asilimia 80, endapo wenye dalili za awali za ugojwa huo wakiwahishwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi na kuanza matibabu ya mapema.

Mwenyekiti wa Bodi ya TLM na mwanzilishi wa taasisi hiyo, Gerald Mongella, akiwa na Daktari Trish kutoka hospitali ya muhimbili.

Watoto zaidi ya 600 waliopatiwa matibabu kwa mwaka 2011 hadi 2018, asilimia 50 hadi 60 wamepona ikiwa ni asilimia 20 ya watoto zaidi ya 2,000 ambao hawajafika hospitali kwa ajili ya matibabu.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu wa Mipango kutoka Taasisi ya Tumaini la Maisha (TLM), Lilian Ndyetabula, wakati wa tamasha la uchagiaji wa huduma za matibabu na elimu kwa umma juu ya magojwa ya saratani kwa watoto.

Alisema kuwa TLM ni taasisi isiyo ya serikali inayofanya kazi kwa karibu na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha saratani kwa watoto na

ilianzisha mwaka 2011 na wazazi wa watoto wenye saratani, madaktari, na wafanyabiashara lengo likiwa ni kutatua changamoto ya watoto wanasumbuliwa na ugonjwa huo kuchelewa kufika hospitali kupatiwa matibabu na kuokoa maisha yao.

“Tulivyokuwa tunaanza tuliwafikia watoto zaidi ya 600 na kati yao asilimia 50 hadi 60 wamepona na kwa hao wanaofika hospitali ni asilimia 20, hivyo tunakadiria watoto zaidi 2,000 hawajafika hii inamaanisha bado kuna kazi kubwa baadaye,” alisema Ndyetabula.

Aliongeza kuwa kwa kipindi hicho watoto wengi walikuwa wanafikishwa hospitali wakiwa wamechelewa na wamepita kiwango cha matibabu na hivyo hupelekea wengi wao kupoteza maisha.

Alisema katika kupunguza changamoto hiyo, wameanzisha mpango mkakati kwa mwaka 2019-2025 wa kuwafikia watoto popote walipo na kuhakikisha hata kama mtoto anasafirishwa kutoka mkoani kwenda Muhimbili afike kwa wakati na kuanza matibabu.

“Katika mpango huu tumeanza kushirikiana na Hospitali kama Bugando, KCMC, Mnazi Mmoja Zanzibar, Mbeya na Dodoma kwa kuweka vituo ambapo wazazi wanaweza kuwapeleka watoto katika hospitali hizo kuanza matibabu ya awali, lakini tunataka tufike hata chini zaidi hadi kwenye zahanati, ambapo huko ndio wanawaona watoto kwa mapema, kwani mzazi wa kijiji sehemu ya kwanza atakayompeleka mtoto ni zahanati,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TLM na mwanzilishi wa taasisi hiyo, Gerald Mongella, alisema saratani kwa watoto inatibika, hivyo wazazi wasikimbilie njia ambazo sio rasmi katika kutafuta matibabu ya watoto wao badala yake wawapeleke hospitali kwa uchunguzi zaidi.

Kwa upande wa Fatuma Heri, ambaye amepona saratani ya shingo, alisema kuwa alipata ugonjwa huo mwaka 2009 na baada ya kufanyiwa vipimo katika hospitali ya CCBRT aligundulika kuwa na saratani ya uvimbe shingoni.

“Namshukuru Mungu kwa kuniponya saratani kwani nakumbuka 2009 nilitokewa na uvimbe kwenye shingo, wazazi wangu walinipeleka CCBRT na nikatolewa nyama kwa ajali ya kufanyiwa kipimo na baada ya majibu nikagundulika kuwa na saratani ya uvimbe shingoni,” alisema Fatuma na kuongeza kuwa;

“Baada ya kugundulika nilianza matibabu, dawa nilizokuwa natumia zilikuwa zinasababisha nanyonyoka nywele na kutapika nawashukuru TLM na Dk. Kaijage kwani niliambiwa mambo mengi sana kuwa ukutumia mionzi hutozaa mara utakufa lakini mimi mpaka leo nipo hai na nimepona,” alisema.

Habari Kubwa