‘Suluhisho ukatili wa kijinsia lipo kwa wanaume’

03Aug 2020
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
‘Suluhisho ukatili wa kijinsia lipo kwa wanaume’

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya ukatili wa kijinsia Kawie Social Development Foundation (KASODEFO), mjini Maswa, mkoani Simiyu, limesema suluhisho pekee la kukomesha vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto lipo kwa wanaume.

Limesema licha ya serikali na wadau wengine kuendelea kupambana na janga hilo ambalo limeendelea kuwanyima haki za msingi wanawake, litatatuliwa endapo wanaume watashirikishwa katika kupiga vita jambo hilo.

Akiongea na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya kilimo na sherehe za wakulima (Nanenane), kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nyakabindi mkoa wa Simiyu, Meneja mradi wa shirika hilo, Marius Isavika, alisema wenyewe ndiyo wenye uwezo wa kumaliza tatizo hilo.

Isavika alisema kuwa shirika limeona kuna haja kubwa ya wanaume kushirikishwa kwenye mapambano hayo.

Alisema mradi huo walioanza kuutekeleza toka mwaka 2016 chini ya ufadhili wa Shirika la Legal Service Facility (LSF), wamebaini kuwa wanaume hawashirikishwi hali ambayo imesababisha matukio hayo kuendelea kuwapo.

“Mashirika mengi tumeona yamekuwa yakiwashirikisha waathirika pekee (wanawake) katika kupiga vita tatizo hili, lakini ukweli ni kwamba tunakosea, lazima wanaume washirikishwe kila hatua ili waweze kutatua matatizo yao wenyewe,” alisema Isavike.

Pia alisema serikali na wadau wengine wabadalishe mfumo kwa sasa na kuanza kuwajumuisha wanaume ili waweze kutambua wanachowafanyia wake zao au watoto wao ni unyama.

Mratibu huyo alisema katika kutekeleza mradi huo, wamegundua kuwa vitendo vimeendelea kuwapo ingawa vinapungua kutokana na wanawake wengi kuanza kutambua haki zao na wapi wapekele matatizo yao.

Alisema katika Mkoa wa Simiyu, wanawake wengi hawawezi kumiliki ardhi wala uchumi wa familia, kazi kubwa kwao ni kuzalisha, lakini kwenye haki ya kutumia walichozalisha hawana.

“Wengi hawajui kama ni haki yao kumiliki ardhi, uchumi wa familia, hawajui kama wana haki kwenye mali wanazozalisha, kati ya kesi 10 ambazo tumekuwa tukipokea, nane zinahusu ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi,” alisema Isavike.

Mratibu huyo alisema shirika hilo limeshiriki maonyesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kupambana na ukatili ikiwa pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa wenye matatizo.

Aliwataka wananchi wote wa mkoa wa Simiyu na mikoa jirani kufika kwenye banda hilo kwa ajili ya kupata elimu ikiwa pamoja na kupewa msaada wa kisheria kwa wenye matatizo mbalimbali yanayohitaji msaada wa sheria.

Habari Kubwa