“Hakuna uhamisho kwa mtumishi aliyeharibu kituo chake cha kazi”

04May 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
“Hakuna uhamisho kwa mtumishi aliyeharibu kituo chake cha kazi”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu, amesema mtumishi wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (TAMISEMI) atakayeharibu katika kituo chake cha kazi hatamruhusu kuhama isipokua atamuwajibisha akiwa katika kituo chake cha kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo katika ziara yake wilayani Chemba mkoani Dodoma kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na kamati ya fedha  pamoja na menejimenti ya halmashauri  hiyo.

“Sitaruhusu  mtumishi aharibu Chemba kisha ahamishiwe Kongwa, niwahakikishie kuwa nitamshughulikia akiwa hapa hapa Chemba na nikibaini ana hatia ntamchukulia hatua stahiki” amesema Ummy.

Ameongeza kuwa watumishi wa TAMISEMI wamezoea kufanya ubadhirifu wa miradi ya maendeleo haswa katika Elimu, Afya na Barabara na wakishaona mradi haujakamilika au unatuhuma anahama. "Sio wakati wa Uongozi wangu hakuna atakayehama kukwepa tuhuma," amesema na kuongeza;

“Na hapa Chemba wote waliohama sababu ya kutokukamilisha miradi ya maendeleo kama Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya watarudi  kuja kujibu tuhuma zao” amesema.

Habari Kubwa