“Marufuku hospitali za umma, binafsi kulipisha chanjo ya corona"

30Jul 2021
Yasmine Protace
DAR ES SALAAM
Nipashe
“Marufuku hospitali za umma, binafsi kulipisha chanjo ya corona"

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa angalizo kwa wasimamizi wa chanjo kutolipisha watu fedha kwani chanjo hizo ni bure.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi wakati wa usambazaji  wa chanjo hizo kwenda mikoa mbalimbali nchini tukio lililofanyika bohari kuu ya dawa MSD, Kurasini Dar es salaam.

Akitoa rai kwa wasimamizi, Prof. Makubi, amesema utoaji wa chanjo hizo kwenye hospitali za Umma na binafsi utatolewa bila kulipisha gharama za chanjo.

"Naelekeza kwa huu mgao wa Covax Facility ni marufuku Hospitali za umma au binafsi kulipisha Wananchi gharama yoyote katika zoezi hili la chanjo na lifanyike kwa uadilifu na kwa haki kwa walengwa wa sasa." amesema Prof. Makubi.

Ameongeza kuwa, pamoja na serikali kufanikisha upatikanaji wa chanjo hizo na kuanza kuchanja Wananchi, Wizara ya afya inaendelea kuwashauri wananchi kujikinga na UVIKO-19.

"Kwa kuzingatia kanuni za UVIKO 19, tunapaswa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali za mita moja au zaidi, kuepuka misongamano na kufanya mazoezi.

Aidha, amesema ugawaji wa chanjo umezingatia taarifa ya visa vya wagonjwa waliohisiwa kuwa na UVIKO-19, idadi ya walengwa kwa kundi la kipaumbele pamoja na idadi ya chanjo zilizopatikana kwa sasa.

Katika hatua nyingine serikali kupitia TMDA, Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa na Vyombo vingine vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa chanjo za Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani. 

Prof. Makubi amebainisha kuwa, kutokana na Mwongozo wa Chanjo wa Taifa dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19, Shirika la Afya Duniani (WHO), maelekezo ya Covax Facility na upungufu wa uzalishaji wa chanjo toka viwandani, Chanjo hizo kwa sasa zinatolewa kwa kufuata vipaumbele vya makundi yenye uhitaji mkubwa.

"Makundi ambayo yataanza chanjo ni pamoja na: Watumishi wa sekta ya Afya, Watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na Watu wenye magonjwa. Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza, uchanjaji kwa makundi yote nchini ni wa hiari au huru kwa kila mwananchi.

Kwa kuwa chanjo zilizopokelewa kwa sasa hazitoshelezi walengwa wa makundi yote nchini, makundi mengine yatapata chanjo katika awamu inayofuata, mara zitakapowasili." amesema Prof. Makubi.

Hadi sasa Serikali inategemea kutoa chanjo kwa makundi yanayolengwa kuanzia Agosti 3,2021, siku ya Jumanne, katika vituo 550 vya kutolea huduma katika mikoa yote ya Tanzania bara ambapo Orodha ya vituo hivyo inapatikana pia katika tovuti ya wizara; www.moh.go.tz. 

Wananchi wote walengwa, wanaotaka kuchanjwa kwa hiari yao, huku wakitakiwa; kujihakiki kama wapo ndani ya makundi matatu ya walengwa kwa sasa.

"Mlengwa atakayepata chanjo kuandaa kitambulisho cha Kazi, NIDA, Leseni ya Udereva, Mpiga kura, Pasi ya Kusafiria au kitambulisho chochote kinachotambulika kisheria.

Kufanya 'booking' ya siku ya kuchanjwa kwa kutumia mtandao ndani ya simu/Computer (online) yako kupitia https://chanjocovid.moh.go.tz au kwa kwenda moja kwa moja kwenye kituo na kujisajili kuanzia Jumatatu tarehe 2 Agosti 2021." amesema Prof. Makubi.

Pia ameongeza kuwa, mlengwa atatakiwa kujaza fomu ya uhiari wa kuchanjwa, Ambapo Wizara inaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini, kukamilisha matayarisho yote muhimu kwa utoaji wa chanjo, ili ifikapo tarehe 03 Agosti 2021, utoaji wa chanjo uwe umeanza katika vituo vilivyoainishwa katika mikoa.

Kutokana na uhitaji na mipangilio ya Mkoa husika, wanaweza kuongeza idadi ya vituo ili kupunguza msongamano katika vituo. Aidha, katika zoezi hili, wananchi, watasajiliwa katika mfumo wa Taifa wa Chanjo na watapatiwa cheti baada ya kuchanjwa.

Habari Kubwa