“Msikurupuke kununua ardhi Dodoma mtanunua makaburi’

17Jan 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
“Msikurupuke kununua ardhi Dodoma mtanunua makaburi’

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, amewatahadharisha wananchi kutoka mikoa mbalimbali wanaokimbilia kununua ardhi isiyopimwa katika Jiji hilo, kuwa makini kuuziwa maeneo ya makaburi.

Alitoa tahadhari hiyo wakati wa kikao kilichowakutanisha wakuu wa taasisi za kiserikali za jiji hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alikuwa akipokea taarifa ya mipango ya upelekaji huduma kwenye maeneo ya uwekezaji na yanayojengwa kwa kasi jijini humo.

Alisema hivi sasa kuna wimbi la watu kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, wanakimbizana maporini kununua ardhi ambayo haijapimwa.

Mafuru aliwataka watambue kuwa Jiji la Dodoma lina ramani yake ya mipango miji ya miaka 20 na hakuna ardhi ambayo haina matumizi.

“Msikurupuke kununua mtanunua makaburi, msikurupuke mkanunua mtanunua msitu, bahati mbaya sana kuna wataalamu juzi walikuwa wanazungumza wakadhani siwasikii wameshanunua chanzo cha maji Makutupora hiyo imekula kwao,” alisema Mafuru na kuongeza:

“Waje waulize kabla ya kufanya maamuzi yoyote ya ardhi, waje tuangalie, ununuaji wa holela wa Jiji la Dar es Salaam au Mwanza kwa Dodoma ni ngumu, master plan (mpango mji) tuliyonayo ni ya miaka 20 na ndiyo kwanza tupo mwaka wa kwanza,” alisema Mafuru.

Alisema kwa sasa kuna upimaji unaendelea kwenye maeneo mbalimbali na ifikapo Juni, mwaka huu Jiji la Dodoma litakuwa limezifikia kata zote 41 katika upimaji wa maeneo, ili wananchi wajenge kwenye viwanja vilivyopimwa.

Kadhalika, alisema madalali wa ardhi waliopo Jiji la Dodoma wengi wao ni wataalamu wa ardhi wastaafu waliokuwa kwenye Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), wana taarifa lakini ambazo siyo za kweli.

“Kabla hujanunua kiwanja chochote uje kuangalia kwenye mfumo inamsoma nani, ili tukujibu endelea, lakini tatizo lipo wateja wetu wengi wanakuja kuangalia wakati walishalipa inakuwa kesi.”

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Binilith Mahenge, aliwataka wananchi kuzingatia maelekezo ya Mkurugenzi huyo, kujiridhisha kuhusu uhalali wa eneo husika.

Dk. Mahenge alisema: “Kwenye ujenzi holela msiweke alama ya ‘X’ bomoeni kabisa maana mnapoweka alama ya ‘X’ wao wanaendelea na mwisho wa siku nyumba inasimama mnapelekana mahakamani, kama amekosea ondoa mara moja.”...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

 

Habari Kubwa