… Mhagama aagiza mfumo mpya vibali kazi

10Apr 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
… Mhagama aagiza mfumo mpya vibali kazi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Tixon Nzunda kuhakikisha mfumo wa utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni unaanza kufanya kazi kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Sambamba na hilo, Waziri Mhagama amewataka watumishi wa ofisi yake kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa kwa ufanisi, kwamba hatosita kuwachukulia hatua.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na watendaji wakuu wa sekta zilizopo katika wizara yake jijini hapa, kueleza kwamba kuanza kwa mfumo huo kutasaidia kuondoa mianya ya rushwa.

“Katibu Mkuu nilishatoa maelekezo haya, siku iliyopangwa mawaziri kutoa mawasilisho ndiyo siku ambayo Rais alitupa mshangao wa mabadiliko ya baraza, lakini tangu hapo hakuna aliyekuja kuulizia,  tulitakiwa tuwe tumeshazindua mifumo huo, sasa nataka nipate maelezo ni kwa nini mfumo huo hatuuzindui,” alisema Mhagama na kuongeza;

“Zipo taarifa nazisikia kuwa bado kuna vitu vinakwamisha lakini wala siyo sababu ya kutufanya tusifanikishe jambo hilo la muhimu sana, sasa sijui anasubiriwa waziri au manaibu ndiyo waseme tena, huu siyo utaratibu mzuri, kila mtu asukumwe kufanya kazi, tuache utendaji wa mazoea, mimi ningependa mara tunapomaliza bajeti yetu, tumpe zawadi waziri mkuu kwa kuanzisha mfumo huu ambao unaenda kutatua kero,”alisisitiza Waziri Mhagama.

 Waziri Mhagama alisema: “Tunajua wapo mawakala wengi wanakwenda kwa waajiri wakijifanya wanaweza kuwasaidia kupata vibali na wanachukua fedha na hapo inaonekana ofisi ya waziri mkuu, sasa ni vyema tujitoe kwenye hii taswira”.

Aidha, aliomba kukutanishwa na maofisa rasilimali watu kwenye kampuni kubwa zote ili ajue changamoto zao na shida wanazopata.

Akipokea maelekezo hayo Katibu Mkuu Nzunda, aliahidi kuyatekeleza kwa kusimamia misingi mitatu ambayo ni weledi, uadilifu na bidii ya kazi.

Nzunda alisema: “Mimi siyo mtu wa mchakato napenda kazi itoe matokeo haraka na nitafanya hivi kwa kuzingatia katiba, sheria, taratibu na mifumo ya utendaji kazi”.

Habari Kubwa