…Machinga wapangwe, wasibugudhiwe

14Sep 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
…Machinga wapangwe, wasibugudhiwe

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewaagiza wakuu wa mikoa kuchukua hatua za kuwapanga vyema wajasiriamali wadogo maarufu kama ‘machinga’ bila uonevu.

Akizungumza kwenye uapisho wa mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ikulu jana, Rais Samia alisema serikali imetoa fursa kubwa kwao kufanya biashara ili kujipatia kipato.

“Watu hawa wamekuwa wakifanya kazi kwenye maeneo tofauti tofauti, wakuu wa mikoa wanawapanga, wakuu wa wilaya wanawapanga, lakini pia watu wamepumzika kiasi ambacho watu hawa sasa wameenea kila mahali mpaka kwenye maduka wao wanaziba, wanauza mbele.”

“Mpaka sasa wenye maduka baadhi yao wamepata mtindo wa kutoa bidhaa zao ndani na kuwapa machinga kuuza kwasababu watu hawaingii ndani, lakini kitendo hiki kinatukosesha kodi kwasababu machinga halipi kodi, lakini mwenye duka anatakiwa kulipa,” alisema.

Aliwataka wakuu hao kuchukua hatua za kuwapanga vyema na kuonya anayoyaona kwenye runinga ya ngumi, kupigana, kufukuzana, kuchafuliana na vitu kumwagwa, hataki kuyaona.

Alisema hatua hizo zichukuliwe vizuri na kuwapanga vyema bila kuudhi wenye maduka wala machinga.

“Niwaombe sana ndugu zangu wakuu wa mikoa mnaonisikia na wale wanaonisikia kupitia runinga wachukue hatua zinazostahiki bila kuleta vurugu, fujo na uonevu,” alisema.

Alitoa wito kwa machinga au wajasiriamali wafuate sheria na kanuni zilizopo na wajitahidi kufuata yale wanayopangiwa na wakuu wa mikoa na wilaya.

Kuhusu viongozi walioapishwa, Rais Samia aliwataka walioapishwa kufanya kazi kwa umahiri mkubwa katika maeneo yao kwa lengo la kutoa huduma stahiki kwa wananchi nasi vinginevyo na yeye ataendeleza kazi ya marekebisho.

“Nimeanza na mabadiliko kwenye muundo wa wizara mbili iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo sasa inabaki kuwa Sanaa, Utamaduni na Michezo na nimechukua Habari nimeipeleka iliyokuwa mawasiliano na Teknolojia ya Habari.”

“Nimefanya hivyo kwasababu Wizara ya Habari, Teknolojia ya habari ili iwe kamili yale maneno habari yote yawe huko na nadhani ikikaa hivi yatakaa vizuri, kilikuwa kilio cha muda mrefu cha watu wa sekta ya habari walipenda idara ile iwe pale,” alisema.

Alisema wizara hiyo ni nzito kidogo ingawa utekelezaji wa mambo yake ulikuwa unachukuliwa kwa wepesi na kumtaka Dk. Ashatu Kijaji kujipanga vizuri.

Kuhusu Wizara ya Ulinzi, alisema kulikuwa na mila iliyojengeka kuwa ni lazima iongozwe na mwanamume mwenye misuli bila kutambua kuwa waziri kwenye wizara sio mpiga mzinga wala mbeba bunduki.

“Waziri kazi yake ni kusimamia sera na utawala wa nikaamua dada yetu Dk. Stergomena Tax nimpeleke huko si kwasababu tu ya kuvunja mila, lakini kwasababu ya upeo wake mkubwa alioupata akiwa SADC.”

“Kipindi chote tukienda SADC alikuwa anasimamia vyema mambo yote ya usalama ndani ya kanda na alikuwa na upeo mkubwa ndani ya Afrika Mashariki kwa hiyo kwa uzoefu alioupata katika sekta ya ulinzi atakwenda kutusaidia huko.”

“Yeye anajua vyema askari waliopo Msumbiji, DRC Kongo kwanini wapo huko mifumo yao inavyobadilika haki zao na mambo yote anajua na nimehisi atamsaidia vizuri CDF katika upande huo,” alisema.

 

Alisema anaamini watafanya vizuri na kwamba uteuzi wao hauna maana kwamba wao ni wazuri kuzidi wote waliokuwapo.

“Uzuri wenu utaonekana katika utekelezaji wa majukumu yenu, kwasababu hata tuliowachagua awali walikuwa wazuri pia mtakavyotekeleza ndio uzuri wenu utakavyoonekana, kwangu mimi ninachotaka kuona ni matokeo sitaki kuwaona kwenye TV tu mnafanya hili mnafanya lile nataka kuona matokeo kwa wananchi,” alisema.

Aliwataka kama wakiona kuna haja ya kufanya marekebisho katika mambo watakayoyakuta wasiwe waoga kuwaeleza viongozi ili kufanya marekebisho na kusisitiza anataka kuona matokeo.

“Ninaposema nataka kuona matokeo sio kwa nyie wapya tu hata wazamani na wenyewe nataka mjipange upya tuone mnafanya nini mnatoa huduma gani kwa wananchi,” alisema.