10 mbaroni tuhuma za wizi wa umeme

22Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
10 mbaroni tuhuma za wizi wa umeme

SHIRIKA la umeme  Tanzania (Tanesco) mkoa maalum wa Temeke, limewanasa wateja 10  waliokuwa wanatumia umeme wa wizi baada ya kuchezea mita za shirika hilo za luku.

Wateja hao walinaswa wakati wa operesheni ya siku tatu ya kukagua mita zao za  luku iliyoendeshwa na shirika hilo kwa lengo la kubaini wateja wanaotumia umeme wa wizi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza operesheni hiyo, katika mkoa huo maalum wa Temeke, Mhandisi Mkuu Mdhibiti Upotevu wa Mapato ya shirika hilo kutoka Makao Makuu, Mposheleye Mwasenga, alisema operesheni kama hiyo haitaishia Temeke bali ni ya nchi nzima.

Mwasenga alisema wateja wao hao, ambao wamewanasa katika operesheni hiyo wamewafungulia kesi katika kituo cha polisi kati kwa hatua zaidi za kisheria.

Alisema kuanzia sasa hawatamkamata mwizi wa umeme, bali wataishia kumkatia umeme na kumpiga faini tu, lakini ni lazima wamfikishe polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

“Tumeamua kuvalia njuga suala la wateja wetu wanaotumia umeme wa wizi, hivyo kila tutakayemkamata mbali ya kumkatia umeme, pia ni lazima tumfikishe polisi kwa hatua zaidi za kisheria, maana shirika linashindwa kupata mapato yake inavyotakiwa ili lijiendeshe vizuri kutokana na wajanja wanaochezea mita zetu za luku na matokeo yake kutumia umeme wa bure,” alisema Mwasenga. 

Habari Kubwa