10 walivyonaswa wakiwa na silaha

12May 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
10 walivyonaswa wakiwa na silaha

JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, linawashikilia watu 10 kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa.

Mmoja wa watuhumiwa hao, Bushiri Ally (29) mkazi wa Tandika, alikutwa na silaha ambayo baada ya kuhojiwa alidai aliiokota barabarani Tandika mtaa wa Mteja mwaka 2014 na kuitumia kwa matukio ya uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Mohamed Ismaili (18) mkazi wa Tandika, Issa Saidi (19) mkazi wa Yombo na Mlekwa Ally (18) mkazi wa Tandika.

Aliwataja wengine kuwa ni Shabani Nassoro (17) mkazi wa Tandika na wengine watano ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Aprili 29 saa sita usiku maeneo ya Tandika Foma, baada ya askari wa doria kulitilia shaka gari namba T 401 CLF aina ya Toyota Alteza, rangi ya fedha.

Alisema baada ya kulikamata gari hilo, waliwakuta watu watano na walipofanya upekuzi walikuta bastola aina ya Browning yenye namba N635BRE ikiwa na risasi mbili ndani ya magazine.

Kamanda Mambosasa alisema katika tukio lingine, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kukutwa na bastola mbili na risasi 16, nyundo moja na bisisi tatu, vilivyokuwa vikitumika katika matukio ya wizi wa magari.

Alisema katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kuliokoa gari la mkazi wa Mbezi Makondeko, Remmy Wilbard ambalo aliibiwa nje ya geti lake huko Makondeko na baadaye majambazi hao kukutwa Sinza wakiwa katika jaribio la kuliuza.

Alisema baada ya Wilbard kufika nje ya geti la nyumba yake akiwa na gari aina ya Toyota Noah namba T681 DJM rangi ya fedha, alishuka na kuvamiwa na watu watatu wakiwa na bastola, silaha za jadi na kumpora.

Alisema kati ya majambazi hao, wawili walikutwa Sinza Kumekucha wakiwa katika jaribio la kuliuza na walipobanwa waliwataja wenzao watatu.

Alisema upekuzi uliofanywa kwa watuhumiwa hao ulifanikisha kukamata bastola ambayo haijatambulika aina yake yenye namba AK-0383 TZCAR 71414 iliyokuwa imefichwa ndani ya kabati la nguo.

“Upekuzi kwenye nyumba ya mtuhumiwa mwingine ulifanikisha kupata bastola aina ya Beretta U.S.A Corp Acookeer MD ikiwa imefutwa namba na risasi sita ndani ya magazine, watuhumiwa hawa walikiri kujihusisha na wizi wa magari na uhalifu wa kutumia silaha,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema kwa muda wa wiki tatu wamefanikiwa kukusanya Sh. 1, 563,082,500 kwa makosa ya barabarani.