138 waishi chini ya miti, mahema

05Jan 2017
Margaret Malisa
KIBAHA
Nipashe
138 waishi chini ya miti, mahema

ZAIDI ya wakazi 138 wa Umoja wa Wakulima Kazamoyo Kata ya Soga Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini, hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomolewa na uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Wananchi hao wameamua kuishi chini ya miti na wengine kwenye mahema kwa kipindi cha miezi mitatu sasa huku wagonjwa, watoto na wazee wakipata adha na usumbufu mkubwa.

Uongozi wa Halmashauri ulifikia hatua ya kubomoa nyumba hizo baada ya kutoa notisi ya siku 60 wananchi hao zaidi ya 622 wahame katika shamba hilo walilokuwa wakilitumia kwa kilimo na makazi zaidi ya miaka saba.

Awali, shamba hilo lilikuwa likimilikiwa na mwananchi mmoja kabla serikali haijalichukua.

Katibu wa umoja huo, Athumani Rashid, alisema wameshindwa kuondoka katika eneo hilo ambalo wamekuwa wakilitumia kwa muda mrefu baada ya kumwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuomba serikali iwatambue kwa kuwapimia ardhi hiyo kwani hawana mahali pengine pa kuishi.

Alisema Waziri Lukuvi kupitia kwa Kamishna wa Ardhi, aliwajibu barua yao na kuwaruhusu waendelee kukaa katika shamba hilo hadi hapo halmashauri itakapoanza kupima maeneo kwa ajili ya kuweka mipango miji ndipo na wao watambuliwe na kupimiwa.

"Hatuwezi kuondoka hapa, Waziri wa Ardhi alisema tuendelee kukaa hapa hadi hapo serikali itakapopanga maeneo ya mji na sisi tutapimiwa.

Tumeishi hapa miaka saba, leo tutaelekea wapi? Huu ulikuwa msitu tena wenye wanyama, tukasafisha na kuanza kutumia matokeo yake kulivyokuwa kusafi tunafukuzwa kama wanyama, tunatishiwa mara kwa mara na polisi, na hata kupelekwa mahabusu.

Tunaiomba serikali yetu, Rais wetu aingilie suala hili, tusiondolewe kinyama kama wakimbizi bila kujua hatma yetu," alisema katibu huyo.

Alisema wanashangazwa na uongozi wa halmashauri ya wilaya kuonyesha wazi kuwa wana maslahi na shamba hilo bila hata kujali barua iliyoandikwa na waziri na wameshindwa kutetea wananchi ambao ndiyo waliowaweka madarakani na kuwataka wahame.

Alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tatu Seleman, alisema watu hao walibomolewa nyumba zao kwa kuwa ni wavamizi na waliingia katika shamba hilo kinyume cha utaratibu.

Habari Kubwa