14 wakiwamo wabunge 3 wa Chadema mahakamani

24Mar 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
14 wakiwamo wabunge 3 wa Chadema mahakamani

WANACHAMA 14 wakiwamo wabunge watatu, meya, diwani na wengine tisa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka saba yakiwamo ya kudharau amri halali, shambulio, kuharibu mali na kutoa lugha ya kuudhi kwa jamii.

Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee wa Kawe (kushoto), Esther Bulaya wa Bunda Mjini (wa pili kushoto), na baadhi ya wanachama wengine wa chama hicho, wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kusomewa mashtaka saba. Habari Uk. 26. PICHA: MIRAJI MSALA

Washtakiwa hao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa, Meya wa Ubungo, Boniface Jacobo na Diwani wa Segerea, Patrick Assenga.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Lenatus Mkude, Mkunde Mshanga na Wakili wa Serikali, Ester Martin, uliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Henry Kilewo na Yohana Kaunya.

Wengine ni Kedmon Mhembo, Mshewa Karua, Khadija Mwago, Pendo Raphael, Cedilia Michael, Happy Abdallah na Stephen Kitomari.

Katika shtaka la kwanza, Mkude alidai kuwa Machi 13, mwaka huu katika Gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam washtakiwa wote 14 na wenzao ambao hawapo mahakamani, walikaidi amri halali ya Sajenti John, aliyekuwa na dhamana ya kulinda geti kuu la ngome ya gereza hilo ya kuwataka waondoke.

Mshanga alidai kuwa siku ya tukio la kwanza, washtakiwa wote 14 na wenzao ambao hawapo mahakamani, walifanya mkusanyiko isivyo halali katika Ngome ya Gereza la Segereana kutoa hofu, amani na utulivu kwa majirani.

Shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa siku ya tukio, katika Gereza la Segerea, washtakiwa wote 14 na wengine ambao hawapo mahakamani walishirikiana kufanya uharibifu wa geti kuu la gereza hilo mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Pia, katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa siku ya tukio, Mdee alitamka lugha ya kuudhi ikiwamo kumkashifu Sajenti John wa Jeshi la Magereza huku akimwamuru kufungua geti hilo na kusababisha uvunjifu wa amani.

Vile vile, katika shtaka la tano, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio mshtakiwa Bulaya alitamka maneno ya kuudhi mbele ya Sajenti John huku akimwamuru kufungua geti hilo na kusababisha uvunjifu wa amani.

Martin alidai katika shtaka la sita, siku na eneo la tukio, mshtakiwa Jacobo alitamka maneno ya kuudhi mbele ya Sajenti John akimwamuru kufungua geti hilo na kusababisha uvunjifu wa amani.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa shtaka la saba, siku na eneo la tukio, mshtakiwa Jacobo alimshambulia Sajenti John kwa kumvuta na kumchania shati la sare ya jeshi hilo akiwa anatelekeza majukumu yake kama mlinzi wa gereza hilo.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yao.

Hakimu Shaidi alisema kila mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho na kitambulisho watakaotia saini ya hati ya dhamana ya Shilingi milioni nne.

Mkude alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika upande wa Jamhuri uliomba tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali pamoja na hati ya wito kwa washtakiwa 13 ambao hawapo mahakamani.

Washtakiwa wote walikamilisha masharti hayo kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Aprili 23, mwaka huu.

Habari Kubwa