14 wamfuata Mpemba ndani

07Nov 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
14 wamfuata Mpemba ndani
  • • Ni yule aliyetajwa na Magufuli Maliasili...

SIKU 10 tangu Rais John Magufuli apongeze kikosi maalumu cha kupambana na majangili kwa kufanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa maarufu wa ujangili wa tembo nchini aitwaye Mpemba, imefahamika kuwa idadi ya watu waliokamatwa katika operesheni hyo imefika 15.

Rais John Magufuli akipokea saluti toka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi.

Akiwa katika ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Mpingo House, jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita, Rais Magufuli alimpongeza Katibu Mkuu Meja Jenerali Gaudence Milanzi kwa kumkamata "Mpemba" licha ya jitihada hizo kukutana na vikwazo awali.

Jina la Mpemba, ambalo si halisi la mtuhumiwa, lilikuwa likitajwa kwa muda mwingi wa serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete kuwa kinara wa ujangili wa kuua tembo nchini.

Akizungumza jijini mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema watuhumiwa hao jumla ya 15 walikamatwa na nyara, bunduki.

Prof. Maghembe alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua ofisi mpya ya utoaji visa za kwenda Israel.

Katika hafla hiyo, pia Waziri huyo alidokeza kuhusu kuimarika kwa ushirikiano baina ya nchi hizo katika kukabiliana na ujangili.

“Tumewakamata pamoja na shehena zao, bunduki na vitu vingi," alisema Prof. Maghembe. "Hatukamati bila kuwa na ushahidi wa kutosha, tukishawakamata na mizigo yao na hawawezi kukataa.

"Tutaendelea na hatutaacha kuwakamata kokote waliko.”

Katika ziara hiyo ya kushtukiza katika Wizara ya Maliasili na Utalii Oktoba 29, Rais Magufuli alikuwa amekwenda kuona meno ya tembo 50 yaliyokamatwa, na watuhumiwa wa ujangili huo akiwemo Mpemba.

UTEUZI WA DCI
Mbali na kupongeza kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Rais Magufuli pia alifanya mambo mawili yenye mwelekeo wa kuongeza kasi zaidi katika vita dhidi ya ujangili wa kuua tembo.

Punde baada ya ziara yake hiyo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athumani katika kile ambacho wachambuzi wa masuala ya siasa wanadai ni kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa polisi katika vita hiyo.

Aidha, Rais Magufuli alimteua Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Mwita Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ili kuimarisha zaidi vita hiyo.

Akijibu swali katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari Ikulu, jijini Ijumaa, Rais Magufuli alithibitisha uzito wa uteuzi wa Jenerali wa Waitara kwa kuuliza "nimeweka Majenerali wawili kwa sababu gani? Huwezi tu ukajiuliza?" wakati akijibu swali linalohusu ujangili.

MSALIE MTUME
Waziri Maghembe alisema yapo madai ya baadhi ya watumishi wa serikali kushirikiana na majangili lakini “hatutakuwa na msalie Mtume wala mhali katika jambo hili."

"Hatusamehi mtu yoyote. Tunapambana na ujangili kwenye uwanja mpana.”

Profesa Maghembe alisema waliokamatwa ni sehemu ndogo ya waliokuwa wanatafutwa, na kwamba kampeni ya kutokomeza ujangili nchini inaendelea ili kukabiliana na mtandao wa ujangili huo.

Alisema kwa kushirikiana an Israel wanatarajia kutumia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kupambana na ujangili katika hifadhi na mapori ya akiba.

Alitaja mapori ya akiba na mbuga zenye changamoto ya ujangili kwa kiasi kikubwa kuwa ni Seluous, hiadhi ya taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambako kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu.

“Nawaonea huruma sana wanaofanya ujangili kwa kuwa lazima wakamatwe na vifungo ni virefu.”

Kwa mujibu wa ripoti ya sensa ya Tembo iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) ya mwaka 2014, miaka 50 iliyopita kulikuwa na tembo 300,000, mwaka 2009 walikuwa 109,000 na sasa inakadiriwa ni 55,000, ikiwa ni upungufu wa asilimia 60 ndani ya miaka mitano.

Tanzania kuna hifadhi za taifa 16 na mapori ya akiba 38, ambako tembo hupatikana na ujangili unadaiwa kufanyika zaidi kwenye mapori ya akiba.

Habari Kubwa