2017 hekaheka

01Jan 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
2017 hekaheka
  • *Enzi ‘dili za kupiga hela’ basi tena
  • *Maaskofu Pengo, Mokiwa wanena

NI mwaka wa hekaheka! Hivyo ndivyo yeyote anavyoweza kueleza kwa ufupi kuhusiana na baadhi ya yale yanayotarajiwa kutwaa nafasi nchini katika mwaka mpya ulioanza baada ya saa 6:00 wa usiku wa kuamkia leo.

Katika kufuatilia kwake, Nipashe imebaini kuwa miongoni mwa yale yatakayokuwa gumzo ni pamoja na kupotea jumla kwa ‘dili za kupiga hela’, hivyo kuchangia kuwapo kwa ukata.

Nipashe imebaini vilevile kuwa uhaba wa fedha utaendelea kuwapo mitaani kutokana na hatua kadhaa zilizoainishwa na serikali katika mwelekeo wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha, na ambao utaanza Julai.

Aidha, mwaka huu unatarajiwa kuwa wa hekaheka pia wakati Serikali itakapokuwa ikitekeleza kwa vitendo ahadi zake kadhaa, ikiwamo ya kuanza kwa ujenzi wa reli ya kiwango cha kisasa (standard gauge); uendelezaji wa mradi wa barabara za juu (fly-overs) na uhamasishaji wa matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki (EFD).

Sakata lililoibuliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuhusiana na faru John, ni miongoni mwa mambo yatakayopata nafasi ya mijadala, kama ilivyo kwa kiporo cha sakata la mkataba wa kampuni ya Lugumi na polisi, ambalo mjadala wake uliahirishwa ndani ya Bunge.

“Kama ilivyo miaka yote, mwaka mpya wa 2017 unatarajiwa kuwa na mambo ya kutikisa pia, baadhi yake yakiwa ni pamoja na haya ya ukata wa fedha na pia vita kubwa inayoendelea dhidi ya vitendo vya ufisadi. Ila muhimu kuliko yote ni kuona kuwa taifa linabaki katika hali ya amani na utulivu,” alisema mmoja wa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa na kijamii.

Wakizungumzia mwaka huu mpya, baadhi ya viongozi wa dini walisisitiza juu ya umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika nchi.

Viongozi hao ni pamoja na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa; Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Sheikh wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salam, Alhadi Mussa Salum.

UKATA WA FEDHA
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kutikisa mwaka huu ni kupotea jumla kwa ‘dili’ mbalimbali za kuingiza fedha, zikiwamo zile zilizokuwa zikitunisha mifuko ya baadhi ya watu katika Serikali iliyopita ya awamu ya nne.

Kwa mujibu wa mwongozo kuhusiana na mwelekeo wa bajeti ijayo, uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango hivi karibuni, Serikali itaendelea kubana matumizi kwa kudhibiti safari za nje; semina; warsha; maadhimisho ya siku mbalimbali; ukodishaji wa kumbi binafsi kwa vikao vya Serikali na kusisitiza matumizi ya teknolojia ya video katika kuendesha vikao vya kikazi vyenye kuhusisha wajumbe kutoka mikoa isiyozidi minane.

Aidha, Serikali imedhamiria pia kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya iliyokuwa ikitumiwa na baadhi ya watu kukwepa kodi, hasa bandarini. Hatua zote hizo zinatarajiwa kuongeza ugumu wa upatikanaji wa fedha mitaani.

“Zile dili za kimjini za kuingiza fedha sasa ni kama zinazikwa rasmi. Hali itakuwa ngumu zaidi kwa watu waliozoea kuingiza mamilioni ya fedha kiujanja na matokeo yake, watakaoathirika ni pamoja na raia wema ambao biashara zao zilikuwa zikichanganya kwa kunufaika na fedha hizi…mfano watu wenye baa, hoteli, maduka ya nguo na yadi za magari. Wote hawa wataathirika kwa kukosa wateja waliokuwa wakiwategemea,” ilielezwa na chanzo kimoja.

Kadhalika, matarajio ya serikali ya kutoa kipaumbele cha matangazo yake kwa vyombo vya habari vya umma ni eneo jingine linalotarajiwa kusababisha athari kubwa za kifedha.

Aidha, uhaba mwingine wa fedha mitaani unatarajiwa kuendelea kutokana na serikali kukazia uamuzi wa kutohifadhi fedha zake katika benki za biashara bali Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Hali hiyo inadaiwa kupunguza uwezo wa benki kukopesha wateja wake na hivyo kuongeza ukata mitaani.

Akizungumzia fedha za taasisi za umma kuhifadhiwa BoT juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, alisema uamuzi huo utaendelea na hautositishwa.

“Kwa ufupi fedha hizi za umma zilikuwa zikitumika vibaya na bodi za mashirika… lakini pia zilitumika kuikopesha Serikali fedha zake zenyewe kwa riba kubwa kupitia biashara ya dhamana na hati fungani za serikali,” alisema Dk. Mpango.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa, akaunti ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa benki kuu ni akaunti za kukusanya malipo pekee.

“Akaunti za matumizi bado zipo katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo kupitia akaunti hizo. Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukuma benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za fedha hadi vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kwa kuhudumia kampuni kubwa na wafanyabiashara wakubwa pekee,” alisema Dk. Mpango.

UJENZI FLY-OVERS, RELI
Ujenzi wa ‘fly-overs’ ulianza katika eneo la Tazara, makutano ya barabara za Mandela na Nyerere jijini Dar es Salaam huku Rais John Magufuli akiweka jiwe la msingi. Tayari harakati za ujenzi zilishaanza na hekaheka zake zinatarajiwa kushika kasi zaidi mwaka huu katika mradi huo uliotengewa kugharimu Sh. bilioni 100.

Kadhalika, ujenzi wa reli ya kisasa inayotarajiwa kujengwa umbali wa kilomita 1,219 kutoka jijini Dar es Salaam hadi nchini Burundi unatarajiwa pia kuanza mwaka huu,

Kwa mujibu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) ambayo ndiyo inayosimamia mradi huo, reli hiyo inatarajiwa kujengwa pembeni mwa ile ya zamani na tayari kampuni 40 zimeshajitokeza kuomba zabuni ya ujenzi wake. Wananchi watakaoguswa na mradi huo wanatarajiwa kulipwa fidia kwa kuzingatia sheria za nchi.

MATUMIZI YA EFD
Hili ni eneo jingine la hekaheka kwa mwaka huu. Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Dk. Mpango alisema wataendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) na kudhibiti udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa walipa kodi.

“Hapa tunawaagiza TRA wafanye kaguzi za mara kwa mara kwenye maduka na ofisi zinazotakiwa kulipa kodi na kuwachukulia hatua stahiki wale wanaokuwa wanadanganya kuwa bado hawajapata mashine za EFD na kuonyesha barua za siku nyingi, tena kuukuu kwa lengo la kukwepa kodi,” alisema Dk. Mpango.

UNUNUZI WA NDEGE
Mwaka jana Serikali ilinunua ndege mbili aina ya Bombadier Q400 kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zilizowasili nchini na kuzinduliwa rasmi na Rais John Magufuli Septemba 28, 2016.

Kwa mujibu wa Rais John Magufuli, serikali imeagiza ndege nyingine aina ya Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Juni mwaka huu.

Ndege nyingine mbili aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni mwaka huo.

Dk. Mpango alieleza kuwa, serikali imeshatoa fedha Sh. bilioni 91.533 kwa ajili ya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nne.

MAMBO YA SIASA
Masuala ya siasa, hasa uendeshaji wa mikutano ya vyama ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuendelea kuwa gumzo pia katika mwaka huu mpya, kama ilivyokuwa mwaka jana wakati wapinzani walipokuwa wakivutana na polisi kutaka wapate ruhusa ya kutekeleza haki hiyo. Hata hivyo, mara kadhaa walizuiwa.

SAKATA FARU JOHN, LUGUMI
Agizo la Waziri Mkuu, la kutaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini ukweli kuhusiana na faru John aliyekuwa katika Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha inatarajiwa kuibua hekaheka pia ikiwa ripoti yake itabaini yale yaliyotiliwa shaka kuwa ameuzwa kwa Sh. milioni 200 huku wahusika wakilipwa malipo ya awali ya Sh. milioni 100.

Majaliwa aliibua sakata hilo wakati wa ziara yake mkoani Arusha mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana.

Tayari pembe zinazodaiwa kuwa za faru John zimeshatua kwa Majaliwa na ameamuru ufuatiliaji wa masalia yake baada ya kudaiwa kuwa amekufa ili vinasaba vyake vithibitishe ukweli wa taarifa kuwa alikufa baada ya kuhamishiwa Grumeti, Serengeti mkoani Mara kwa kufuata taratibu zote.

VIONGOZI WA DINI WANENA
Wakizungumzia Mwaka Mpya, baadhi ya viongozi wa dini walisisitiza umuhimu wa kuzingatia amani.

Askofu Dk. Mokiwa alisema ni muhimu kuliombea taifa, lakini pia akashauri kuwa vyama vya siasa viruhusiwe kufanya shughuli zao za kisiasa kwa uhuru, lakini pia vikizingatia kutunza amani na utulivu.

Akizungumza na Nipashe muda mfupi baada ya kukabidhi misaada ya vitanda, magodoro, shuka pamoja na viatu katika Hospitali ya Mwananyamala ya jijini Dar es Salaam, Dk. Mokiwa aliviasa pia vyama vya siasa kuwa na ushirikiano.

Alitaka kuondokana na migogoro ili vyama viweze kufanya siasa ambazo mwisho wa siku zitawasaidia Watanzania kujiletea maendeleo ya kweli.

"Tunajenga nyumba moja hakuna haja ya kugombea fito. Vyama vyote vipewe fursa ya kufanya siasa mwaka 2017 unaoanza kesho (leo)," alisema.

Msemaji wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Bernard James, alisema mwaka 2017 uwe mwaka wa amani na kila mmoja kuzingatia sheria na katiba ya nchi.

Alisema ni vizuri pia kwa Serikali kuimarisha uchumi na kuwawezesha wananchi wote kujitegemea kwa sababu kufanya hivyo ni njia mojawapo nzuri ya kuondoa malalamiko na kudumisha amani na utulivu.

Aidha, Kardinali Pengo alikaririwa akiwatakia kheri Watanzania na kuwataka kumshukuru Mungu kwa kusema ‘ahsante’.

Kwa upande wake, Alhadi Mussa Salum alisema ni vizuri amani ikadumishwa wakati wote ikiwamo mwaka huu na kwamba, njia mojawapo ni kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao kwa uhuru na kuzingatia sheria.

Aidha, aliwataka wanasiasa kuacha kuchukuliana kama maadui bali kuwa na umoja na kuimarisha amani ya nchi.

Habari Kubwa