26 kukamatwa tuhuma za ufisadi wa mabilioni Saccos

15Feb 2020
Gideon Mwakanosya
Ruvuma
Nipashe
26 kukamatwa tuhuma za ufisadi wa mabilioni Saccos

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, ameziagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata viongozi kadhaa wa ushirika waliosababishia vyama vyao hasara ya Shilingi bilioni 1.3

Mndeme ameagiza wenyeviti, mameneja na wahasibu wa vyama vya akiba na mikopo (saccos) 26 wanaotuhumiwa kwa ufisadi wa Shilingi bilioni 1.3 kukamatwa mara moja.

Aliagiza kukamatwa watumishi hao jana alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa vyama na wanachama wake.

Mndeme alikuwa kwenye mkutano wa viongozi na wanachama wa vyama vya akiba na mikopo vya wilaya ya Songea na Namtumbo uliofanyika Songea.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wanachama hao ambayo yalihusiana na wanachama wastaafu kutokupatiwa marejesho ya fedha zao walizokuwa wakiweka akiba.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa baada ya kupata malalamiko mengi,serikali inachukua hatua kwa kumtaka mrajisi msaidizi wa ushirika wa mkoa wa Ruvuma kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo kutokana na kuwapo viashiria vya ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za wanachama.

Alifafanua kuwa vyama vya akiba na mikopo 26 kati ya 124 vya mkoa wa Ruvuma vilifanyiwa ubadhirifu na kilichoongoza kulalamikiwa ni Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu Songea Vijijini ambacho wanachama 77 wanadai milioni 73.1.

Alisema kufuatia hali hiyo aliamuru kukamatwa kwa wenyeviti, mameneja, wahasibu pamoja na viongozi ambao muda wao ulipita.

“Wakamatwe na kuhojiwa ili kufanikisha kupata ufumbuzi wa upotevu wa fedha hizo.” Alisema Mkuu wa Mkoa. Mapema akitoa taarifa ya mikopo na madeni ya vyama vya akiba na mikopo kwa msimu wa mwaka 2018 /2019 mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika wa mkoa wa Ruvuma, Bumi Masuba mbele ya Mkuu wa Mkoa alisema, Ruvuma una vyama vya ushirika 124.

Alisema kati ya hivyo 38 vipo katika hatua ya kufutwa kufuatia agizo la serikali kuvifuta vyama ambavyo havifanyi kazi hivyo Ruvuma inabakiwa na vyama 86.

Alifafanua kuwa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo haviendeshwi kwa ufanisi kutokana na matatizo mbalimbali kama utunzaji wa kumbukumbu za hesabu, kutopatikana kwa viongozi waadilifu, kutotaka kukaguliwa pamoja na uwepo wa madeni lala yasiyolipika kwa kiasi kikubwa.

Yote hayo alisema yameathiri mzunguko wa fedha na kusababisha kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wanachama, wanaolalamikia kukosa huduma na mikopo kwa mahitaji mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Akichangia hoja kwenye mkutano huo,mmoja wa wanachama wa chama cha akiba na mikopo cha changanyikeni Saccos Mustafa Songambele, alisema kuwa sababu kubwa ya kuwapo kwa madeni katika Saccos hiyo ni kutokana na viongozi kukopesha idadi kubwa ya fedha bila ya kufuata utaratibu tena kuwapa fedha watu ambao si wanachama.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Pili Mande, alisema mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, amewakamata watuhumiwa 18 kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Habari Kubwa