500 wapatiwa miguu bandia 

17Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
500 wapatiwa miguu bandia 

WATANZANIA 551 wamepata miguu bandia bila malipo katika kambi ya kutoa huduma hiyo iliyofanyika kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Taasisi ya BMVSS ya India.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo juzi jijini Dar es Salaam, alisema imefanyika kwa mafanikio makubwa.

Alisema kambi hiyo iliendeshwa kwa siku 42 ikiushirikisha pia Ubalozi wa India nchini na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

"Kwa namna ya pekee, niwashukuru wataalamu kutoka India kwa moyo wa upendo wa kujitolea kufanya kazi hii ya kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji wa miguu bandia.

"Vilevile, niwashukuru na kuwapongeza wataalamu wa MOI ambao wameshirikiana na wataalamu kutoka India kuendesha zoezi hili," Dk. Boniface alisema.

Alisema sababu za watu kupoteza viungo ni ajali za barabarani na ugonjwa wa kisukari, huku akiweka wazi kuwa kumekuwa na ongezeko la wahitaji wa miguu bandia.

"Vyanzo vikuu vya watu wengi kupoteza viungo vyao ni ajali za barabarani pamoja na ugonjwa wa kisukari, natoa wito kwa jamii kufuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali.

"Pia kuepuka mtindo wa maisha unaoweza kupelekea  kupata magonjwa ya kisukari, ni muhimu tukafanya mazoezi ili kulinda afya zetu," Dk. Boniface alisema.

Katika hatua nyingine, MOI imeingia mkataba wa ushirikiano wa mafunzo, kubadilishana wataalamu na utaalamu na Taasisi ya BMVSS Jaipur ya India kwa lengo la kuboresha utoaji huduma za miguu bandia nchini.

Mkataba huo ulitiwa saini na Dk. Boniface wa MOI na mwanzilishi na mlezi wa Taasisi ya BMVSS, Dk. Devedra Raj Mehta na kushuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI, Prof. Charles Mkonyi na Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ushirikiano wa Kimataifa wa BMVSS, Satich Mehta.

"Mkataba huu utasaidia sana kwani lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hizi za viungo saidizi na bandia kwa ubora wa hali ya juu ili kuwasaidia hususani wa kipato cha chini ili waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa," Dk. Boniface alisema.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Uhusiano wa Kimataifa BMVSS, Satich Mehta, alisema BMVSS itatoa fursa kwa wataalamu wa MOI kupata mafunzo India bila malipo.

"Tutatoa fursa kwa wataalamu wa MOI kuja kujifunza kwa miezi miwili au zaidi, lengo letu ni kuhakikisha ujuzi zaidi unapatikana hapa MOI na wananchi wengi zaidi wananufaike, hasa wale wa kipato cha chini," Mehta alisema.

MOI imekuwa ikianzisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za matibabu inazotoa.