72 wanaswa operesheni ya Loliondo, wamo raia Kenya

06Jul 2022
Novatus Makunga
ARUSHA
Nipashe
72 wanaswa operesheni ya Loliondo, wamo raia Kenya

OPERESHENI maalum ya siku 10 iliyofanywa na Jeshi la Uhamiaji katika Tarafa za Sale na Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, imewanasa watu 72 walioingia na kuishi nchini kinyume cha sheria.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji (ACI), Hosea Kagimbo.

Jeshi hilo pia limefanya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO) yaliyoko katika tarafa hizo mbili.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji (ACI), Hosea Kagimbo, waliokamatwa ni raia wa Kenya 57, raia wa Ufaransa saba na walowezi  wanane.

Kagimbo alisema kati ya watuhumiwa hao, 30 watafikishwa mahakamani huku 13 wakiachiwa huru ilhali wengine 29 uchunguzi bado unaendelea.

Hata hivyo, Kagimbo alisema zoezi hilo limekabiliwa na vikwazo vya baadhi ya watu kuyakimbia maboma yao na uchunguzi unaendelea wa kuwasaka.

Kamishina Msaidizi wa Uhamiaji huyo alieleza kuwa wamezifikia NGO 10 na walifanya mahojiano ya kina na wafanyakazi wake.

Kufanyika kwa operesheni hiyo kumetokana na agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alipotembelea maeneo hayo Juni 15 mwaka huu wakati wa uwekaji wa alama za mipaka ya Pori Tengefu Loliondo.

Serikali imepunguza ukubwa wa Pori Tengefu la Loliondo kutoka kilometa za mraba 4,000 hadi kilometa za mraba 1,500 huku ikiacha kwa wananchi kilometa za mraba 2,500.

Pori hilo sasa linajulikana kama Pori Tengefu la Pololeti baada ya kupunguzwa ukubwa na kuwekwa kwa alama za mpaka. Pololeti ni jina la mto maarufu na muhimu uliopo ndani ya pori hilo.

Habari Kubwa