9 watumbuliwa serikalini

17Apr 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
9 watumbuliwa serikalini

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amemsimamisha kazi Meneja wa Kitengo cha Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dk. Milali Machumu, kutokana na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini dosari katika usimamizi wa kitengo hicho.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

Pia ametangaza kuivunja Bodi ya Wadhamini ya Mamlaka ya Hifadhi za Bahari iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Prof. John Machiwa ikiwa na wajumbe nane.

Hatua hizo zimechukuliwa kutokana na ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17 kubaini udhibiti duni wa matumizi ya rasirimali za bahari katika maeneo tengefu na ukiukwaji na ufuatiliaji wa doria zisizotosheleza katika kukabiliana na ongezeko la shughuli haramu katika hifadhi za bahari.

Ripoti ya CAG iliyowasilishwa bungeni mjini hapa Jumatano, pia ilibainisha kuwa kamati za uhifadhi hazikuundwa kwenye vijiji vyote vilivyopo kwenye maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini hapa jana kuzungumzia hoja zilizoibuliwa na CAG na kuelekezwa kwa wizara yake, Mpina alisema serikali imedhamiria kulinda rasirimali za nchi, hivyo alitoa wito kwa idara na taasisi zilizopo kwenye wizara yake kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo ya serikali.

Kabla ya kutangaza kumsimamisha kazi Dk. Machumu, waziri huyo alisema taarifa ya CAG kuhusu ukaguzi wa ufanisi katika usimamizi wa hifadhi za habari na maeneo tengefu imebainisha udhaifu katika usimamizi wa hifadhi za bahari na maeneo tengefu kutokana na udhaifu wa menejimenti na bodi ya wadhamini inayosimamia kitengo hicho.

Kutokana na kusimamishwa kwa Dk. Machumu, Mpina alimwagiza Katibu Mkuu wa wizara yake kuunda kamati ya uchunguzi kuhusu utendaji wa meneja huyo.

UTEKELEZAJI HOJA

Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, alisema utekelezaji wa hoja zilizoibuliwa kwenye ripoti ya CAG ikiwamo uwapo wa viwatilifu ambavyo havijasajiliwa umeshaanza.

Alisema changamoto hiyo imetokana na kuwapo kwa uingizaji haramu wa viwatilifu hivyo kwa sababu ya urefu wa mipaka ya nchi na uchache wa vituo vya ukaguzi.

Dk. Tizeba alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kukamata vyombo vya usafiri vinavyotumika kuingiza viwatilifu kinyume cha sheria.

"Wizara inaendelea kuongeza vituo vya ukaguzi mipakani na kuweka wakaguzi, kuimarisha ukaguzi wa kushtukiza katika maduka ya pembejeo za kilimo na kuwachukulia hatua za kisheria watakaobainika kukiuka utaratibu," alisema.

Kuhusu hoja ya CAG juu ya uwapo wa wakaguzi mipakani wasiokuwa na ujuzi wa kutosha kusimamia viwatilifu, Dk. Tizeba alisema serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa waajiriwa wapya na wazamani, akibainisha kuwa kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, itatoa mafunzo ya utaalamu wa ukaguzi wa viwatilifu kwa wataalamu 100.

Pia alisema serikali itaendelea kutoa mafunzo ya taaluma maalum ya viwatilifu na mabomba ya kunyunyizia kwa wauzaji wa viwatilifu na wataalamu wa kilimo kwa kushirikiana na halmashauri zote.

Habari Kubwa