Aagiza kuswekwa ndani wanywaji pombe asubuhi

18Mar 2019
Friday Simbaya
IRINGA
Nipashe
Aagiza kuswekwa ndani wanywaji pombe asubuhi

DIWANI wa Kata ya Mwanagata katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Nguvu Chengula, ameagiza kukamatwa watu wote wanaokunywa pombe za kienyeji nyakati za kazi.

Amesema anaamini ulevi kupita kiasi ni miongoni mwa mambo yanayochangia kukwamisha maendeleo katika jamii, akieleza kuwa amekuwa akisikitika kuona baadhi ya wananchi wanakunywa pombe asubuhi badala ya kufanya kazi za kuwaongeza kipato.

Chengula alitoa agizo hilo jana alipozungumza na wamiliki wa nyumba katika kata yake alipohitaji kujua idadi ya nyumba na wakazi walioko katika kila nyumba.

Alisema atawakamata watu wote wanaokunywa pombe kwenye vilabu nyakati za kazi kwa kuwa wanakwamisha maendeleo.

Diwani huyo aliwataka wenyeviti na watendaji wa mitaa yote kuhakikisha vilabu vya pombe vyote vinafunguliwa kuanzia saa 10 jioni baada ya watu kumaliza kazi zao.

Alisema wamiliki wa vilabu hivyo wanapaswa kuzingatia agizo hilo vinginevyo wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuwa ndiyo chanzo cha kuwa na vibaka na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi na serikali kwa ujumla.

Alidai kuwa kata yake hiyo inaongoza Manispaa ya Iringa kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU). Halmashauri hiyo ina kata 18.

Alidai kasi ya maambukizo ya VVU inasababishwa na ngono zembe kutokana na unywaji holela wa pombe za kinyeji na matumizi ya dawa za kulevya.

Chengula pia alisema atashirikiana na wataalamu wa Manispaa ya Iringa kufanya operesheni ya nyumba kwa nyumba kukagua vyoo na ikibainika nyumba haina choo, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wahusika.