Abambwa kwa tuhuma za kukutwa na meno ya tembo

06Jul 2019
Gurian Adolf
KATAVI
Nipashe
Abambwa kwa tuhuma za kukutwa na meno ya tembo

POLISI mkoani Katavi wanamshikilia  mkazi wa  Kijiji cha Songambele wilayani Tanganyika kwa tuhuma za kukutwa na meno manne ya tembo na kipande kimoja  akiwa ameyapakia kwenye baiskeli yake.

Kamanda wa  Polisi Mkoa wa katavi, Benjamin Kuzaga, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi majira ya saa 2.30 usiku.

Alisema askari polisi walipata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo anajihusisha na biashara  haramu ya nyara za  serikali ambazo alikuwa anazipata kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Baada ya taarifa  hizo, alisema polisi walianza kuandaa mtego kwa lengo la kumnasa na hatimaye kumnasa akiwa na meno  mazima  manne  na kipande kimoja.

Alisema nyara hizo zilikuwa amezibeba ndani ya mfuko aina ya salfeti akiwa amepakia  kwenye  baiskeli  yake  yenye namba  S7 G 20138 katika barabara ya Mpanda  kuelekea Ikola.

Kwa mujibu wa Kuzaga, mtuhumiwa huyo bado anaendelea kushikiliwa na polisi naupelelezi utakapokamilika, atafikishwa  mahakamani  kujibu  tuhuma zinazomkabili.

Kamanda   Kuzaga  alisema  katika tukio lingine, Masoud  Mbaruku (60), mkazi wa  Kijiji cha  Ruhafe  wilaya ya Tanganyika, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na silaha  aina ya gobore  yenye  namba 424  kwenye mtutu akiwa analimiki bila kibali.

Alisema mtuhumiwa  huyo  alikamatwa na  gobore  hilo juzi majira ya saa 9 alasiri  akiwa  amelificha  ndani  ya kambi ya muda  ya  uwindaji haramu  ndani  ya  hifadhi ya msitu wa Tongwe Mashariki.

Kamanda huyo pia alisema polisi wamewakamatwa watu  wawili katika maeneo tofauti ya  wilaya za  Mpanda na  Mlelewakiwa na  dawa za kulevya aina ya bangi.

 Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Jegi  Lubinza (42)  mkazi wa   Kijiji  cha   Kabunde  wilaya ya   Mlele  akiwa na  bangikete 16 na gramu 25 akiwa  amezificha  ndani  ya nyumba yake  na nyingine  akiwa ameichimbia ardhini  kwenye salfeti.

Alimtaja  mtuhumiwa mwingine  aliyekamatwa kuwa ni  Joseph  Erick (37) mkazi  wa  Kata ya  Itenka, Mpanda aliyekamatwa akiwa  na bangi  kete mbili. Alikamatwa kwenye eneo la  Katente   ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi  akiwa amehifadhi ndani ya mfuko  wa suruali  yake  kwenye  kipande cha gazeti.

Alisema kuwa watuhumiwa hao wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani ili kujibu  tuhuma zinazowakabili.