Abiria Dar walalamika daladala kukatisha ruti

22May 2020
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Abiria Dar walalamika daladala kukatisha ruti

ABIRIA wanaofanya safari kutoa Segerea kwenda Makumbusho, jijini Dar es Salaam, wamelalamikia baadhi ya madereva wa daladala zinazofanya ruti ya njia hiyo kukatisha safari wakati wa asubuhi kinyume na sheria.

Hali hiyo ilibainika baada ya abiria katika kituo cha Segerea jana kulalamikia baadhi ya daladala kuvuruga utaratibu na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa magari hayo.

Jafari Haule, mkazi wa Segerea alisema utaratibu huo wa baadhi ya madereva unasababisha kuwapo kwa mkusanyiko mkubwa katika vituo vya daladala na kuhatarisha usalama wa kiafya wakati huu wa kupambana na ugonjwa wa Covid -19.

“Baadhi ya daladala zinakuja lakini zinageuzia nje ya kituo, zingine zinaingia, lakini hazichukui abiria, kwa zile zinazo chukua utakuta wanasema wanaishia Ubungo wakifika huko wanatangaza tena kuwa wanaenda Makumbusho,” alisema.

Lilian Martin, mkazi wa Segerea alisema hali hiyo inafanyika kwa wiki ya tatu sasa na kugeuka mazoea kwa baadhi ya madereva wakishirikiana na makondakta.

“Tunawaomba maofisa wa usalama barabarani kutusaidia kutatua changamoto hiyo na kuwachukulia hatua ya kisheria watakao wabaini kutekeleza jambo hilo kwa kuwa linasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi,” alisema.

Jonassi Lyaheja, ambaye ni miongoni mwa dereva wa daladala zinazolalamikiwa alipoulizwa kuhusu shutuma hizo, alisema kutokana na agizo la ‘level seat’ vituoni abiria wanapanda na kugeuza na magari.

“Unakuta gari inajaa hata kabla ya kufika mwisho sasa huwezi kuchoma mafuta bila sababu ukizingatia hata kipato chetu cha sasa kimeshuka, ndio maana wakati mwingine tunageuza,” alisema.

Nipashe ilipowasiliana kwa njia ya simu na Kamishna Msaidizi wa Polisi Ilala (ASP), Zuberi Phembera, kuhusu tatizo hilo, alisema atalifuatilia jambo hilo kwa kushirikiana na maofisa wa usalama wa barabarani.

"Sikuwa na taarifa ya suala hilo kabla, lakini nitalifuatilia kwa kushirikiana na maofisa wa usalama wa barabarani," alisema.

Habari Kubwa