Abiria wakwama daraja kukatika

17Jan 2019
Idda Mushi
Kilosa
Nipashe
Abiria wakwama daraja kukatika

MAWASILIANO ya barabara kuu ya Morogoro -Dodoma yamekatika, hivyo watumiaji wa barabara hiyo kushindwa kuvuka upande mmoja kwenda mwingine baada ya kukatika kwa kingo ya daraja la Dumila Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Wananchi wakishuhudia kijiko cha kampuni ya ujenzi ya Yappi, kikirekebisha sehemu ya Daraja la Mto Magole, eneo la Dumila, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, lililoharibika kutokana na maji ya mvua kubwa iliyonyesha jana na kusababisha barabara kuu ya Dodoma-Morogoro kufungwa. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Hii ni mara ya pili tangu kukatika tena miaka mitano iliyopita kutokana na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Januari 16, mwaka huu katika mikoa ya Morogoro, Manyara, Dodoma na Tanga.

Mwandishi wa habari hizi alifika eneo la tukio na kushuhudia foleni ndefu ya magari zaidi ya 500 kwa kila upande iliyosababishwa na kushindwa kupita kwa watumiaji wa barabara kutokana na hatari iliyokuwapo katika eneo hilo.

Eneo la maungio ya kingo na daraja kwa chini ilionekana kukosa kizuizi chochote kwa umbali wa karibu mita 10 isipokuwa kipande cha juu cha lami pekee.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Willibrod Mutafungwa, alisema askari wamejipanga vya kutosha kuwaelekeza magari madogo na mabasi ya abiria kuzungukia barabara ya Iringa kukatiza Melela-Mkata-Kimamba hadi Dumila ambayo ni ya vumbi huku malori yakitakiwa kusubiri kukamilika kwa matengenezo ya dharura.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema hakuna taarifa zozote za madhara ya kibinadamu zilizoripotiwa kujitokeza kutokana na mvua hizo na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa zozote katika mamlaka mbalimbali kuanzia vijiji hadi Mkoa na katika jeshi hilo watakapogundua lolote.

Alisema jitihada zaidi zinafanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa (Tanroads) Mkoa wa Morogoro kurekebisha tuta linalounganisha daraja hilo na barabara ya lami ili barabara hiyo kuu iendelee kutumika baada ya maji kupungua kutokana na kuanzia majira ya usiku wa kuamkia jana maji kuwa mengi na kufunika kabisa daraja hilo.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Morogoro, Mhandisi Doroth Mtenga, alisema awali wiki moja kabla ya athari zilizotokea,walibaini nyufa katika eneo hilo na kumpeleka mkandarasi kufanya matengenezo, lakini wakati akiendelea na kazi mvua kubwa zilisababisha tuta hilo kung'oka kwa chini na wakalazimika kuzuia magari yasiendelee kutumia barabara hiyo hadi wakamilishe matengenezo.

Kuhusu malalamiko ya wananchi kuzuiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) wasichimbe mchanga ndani ya mto huo, likisema ni kuchangia mafuriko ya mara kwa mara kutokana na mto kujaa mchanga, Mtenga alisema wamekuwa wakiondoa mchanga na kama ungekuwa umeachwa athari zaidi zingeweza kutokea pande zote mbili za daraja kwa kuwa shughuli za kibinadamu zimesababisha mchanga mwingi kujaa.

Alisema wanachohitaji ni kufanyika stadi kubwa zaidi na usanifu wa kina katika eneo hilo ili kuangalia ni namna mto huo utaweza kupitisha maji bila kuathiri barabara na kwamba hali ya sasa ya mchanga imesababisha kazi katika daraja hilo kupaswa kuwa endelevu hasa kuondoa mchanga.

Meneja huyo alisema awali maji yalipita juu ya daraja usiku wa saa tisa na kukata pembeni ya daraja kabla athari zaidi kuonekana chini.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, alisema katika kuhakikisha daraja linarudi katika hali yake na kuanza kutumika kama kawaida, wameshirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wataalamu kutoka Tanroads, wanaotengeneza reli ya kisasa (SGR) pamoja na wa kampuni YAPI ya China wanaotengeneza barabara ya Magole Turiani jambo litakalopunguza gharama za matengenezo ya dharura.

“Barabara hii sio muhimu kwa Watanzania pekee bali inaunganisha Tanzania na nchi za maziwa makuu na ni muhimu sana kiuchumi,” Alisema Dk. Kebwe.

Aliwataka wafanyabiashara wa vyakula kuzingatia usafi wa vyakula wanavyouza ili kuepuka magonjwa ya mlipuko kutokana na mrundikano wa watu na kuahidi kazi za ujenzi zitaendelea usiku na mchana hadi njia hiyo ipitike haraka iwezekanavyo.

Baadhi ya madereva wa magari makubwa waliiomba Serikali kuharakikisha matengenezo ili waweze kuendelea na safari huku wenyeji wakitumia fursa hiyo kama njia ya kujiingizia kipato kwa kuvushana kwenye maji kwa gharama ya kati ya shingi 1,000 hadi 3,000.

Januari 2013, kingo za daraja hilo zilikatika pande zote mbili na kusababisha barabara hiyo kushindwa tena kutumika ambapo aliyekuwa Waziri wa Ujenzi kwa wakati huo ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuwaita wahandisi hata waliokuwa likizo na kutoa motisha kwa madereva wakakesha na kutengeneza usiku na mchana eneo hilo kwa siku tatu tu, tofauti na matarajio kuwa kazi hiyo ingetumia zaidi ya wiki moja kukamilika.

Habari Kubwa