Abiria walalamika kushushwa sehemu za wazi 'kuchimba dawa'

17Jan 2022
Pendo Thomas
SINGIDA
Nipashe
Abiria walalamika kushushwa sehemu za wazi 'kuchimba dawa'

Baadhi ya abiria wamelalamika utaratibu wa mabasi yanayofanya safari kutoka Mkoa wa Dodoma kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi kushusha abiria kuchimba dawa katika eneo la wazi na ambalo ni makazi ya watu.

Mabasi hayo yamekuwa yakishusha abiria katika eneo la Kijiji cha Lusilile Kata ya Kintiku wilayani Manyoni bila kuzingatia faragha za abiria huku eneo hilo pia likiwa limepakana na Shule ya Msingi Lusilile

Aidha,  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), imewahi kupiga marufuku utaratibu wa abiria kushuka maporini na kujisaidia.

Sumatra iliwahi kutangaza sehemu maalumu ya kuchimba dawa kwa njia ya Dar es Salaam - Mwanza; ambapo magari yanapitia mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida,Tabora na Shinyanga, ‘dawa itachimbwa’ Msamvu, Gairo kuna hoteli ambayo inahudumia bure, Badueli umbali wa kilometa 3 kutoka Dodoma mjini pia huduma ni ya bure.

Akitoa malalamiko yake leo majira ya saa moja asubuhi wakati tukio hilo, mwanaume mmoja kwa sharti la kutokutajwa jina lake, amesema haiwezekani huu ni udhalilishaji yaani tunashushwa kwenye makazi ya watu mahali ambapo hamna vichaka wala pa kujistili hii haipendezi.

Abiria mwingie ambaye ni mwanamke akiwa anaelekea 'kuchimba dawa' (kujisaidia haja ndogo) alisikika akisema "Hapana hii inapaswa kukomeshwa yaani mazingira tulio shushwa tunalazimika kuchimba dawa kwa kuchanganyikana huku wananchi wanao pita wakituona hapana hii sio sawa kabisa.

"Ni heri tushushwe maeneo yenye vichaka ili kuwe na ufaragha ,nimelazimika kushuka sababu kama nisipo fanya hivyo ni kupata nafasi nyingine mapema hawata kubali kusimamisha gari "amesema.

Mwandishi wa habari hii ameshuhudia mara kadhaa abiria wakishushwa katika eneo hilo kuchimba dawa.

Nipashe ilijaribu kuwatafuta Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), bila mafanikio.

Habari Kubwa