Abiria watashauriwa kuwa makini usafiri wa majini

09Jan 2017
Lilian Lugakingira
BUKOBA
Nipashe
Abiria watashauriwa kuwa makini usafiri wa majini

ABIRIA wanaotumia vyombo vidogo vya usafiri vya majini, wametakiwa kukataa kusafiria vyombo hivyo, ambavyo vinaondokea katika bandari zisizo rasmi, ili kupunguza ajali za majini.

Mbali na kukataa kusafiria vyombo vinavyoondokea katika bandari zisizo rasmi, pia abiria hao wametakiwa kutosafiria vyombo vilivyojaza mizigo kupita kiasi au vinavyosafiri usiku.

Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), David Mziray, wakati wa kikao cha wadau wa vyombo vidogo vya usafirishaji majini, wamiliki wa vyombo hivyo na wamiliki wa bandari na mialo, kilichofanyika katika Manispaa ya Bukoba.

Mziray alisema kufuatia uchunguzi unaoendelea kufanyika kuhusu ajali za majini, imebainika ajali nyingi zinazovihusisha vyombo vidogo vya majini ni ubora usiokidhi viwango, hali mbaya ya hewa, upakiaji wa mizigo na abiria kuzidi uwezo wa chombo.

Nyingine ni vyombo kuendeshwa na wafanyakazi wasio na sifa au uzoefu unaostahili, kusafiri usiku na bila ya kuwa na vifaa vya kuongozea chombo na taa za kuepusha kugongwa na vyombo vingine hasa vikubwa na kukwepa kutumia mialo au bandari rasmi.

Alisema ili kuepuka ajali hizo ni lazima kuhakikisha hakuna chombo kinachoruhusiwa kuanza safari kama hakijakaguliwa na kupewa cheti, hakijasajiliwa au kimepakia kuzidi kiasi.

”Chombo kisicho na mitambo au injini hakiruhisiwi kubeba abiria na hakiruhisiwi kuanza safari kama hakina vyombo vya kuokolea maisha hasa majaketi ya maisha au maboya,” alisema Mziray.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, alisema ni ukiukwaji wa sheria kwa wamiliki wa vyombo hivyo kuvipeleka majini bila kuwa na ubora unaostahili.

”Lakini pia hairuhusiwi chombo hicho kipakie abira kuzidi kiasi, anayefanya hivyo afahamu kuwa akikamatwa atachukuliwa hatua za kisheria, maana anahatarisha usalama na maisha ya wananchi,” alisema Kijuu.

Kijuu alisema pamoja na mambo yote hayo, hatua muhimu katika kuhakikisha usalama wa chombo ni kukijenga madhubuti, ili kihimili hatari za majini.

”Majini kuna vitu vingi mfano mawimbi, upepo na kugonga miamba, kwa hiyo nyenzo za uokoaji zinazolingana na idadi ya watu waliomo ndani ya chombo husika ni za muhimu,” alisema Kijuu.

Habari Kubwa