ACT wataka kamati huru uteuzi viongozi wa NEC

08May 2022
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
ACT wataka kamati huru uteuzi viongozi wa NEC

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema mchakato wa kupata Katiba Mpya unapaswa kuanza sasa badala ya mwaka 2025 huku kikipendekeza kuwapo kamati huru ya uteuzi wa viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji

Katika hotuba yake wakati wa kongamano la pili la Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea Katiba Mpya, jijini Mwanza jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji, alisema kikosi kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan cha kukusanya na kuchambua maoni ya wadau wa siasa kimetoa ripoti yake ya awali.

Alisema sehemu ambayo hawakubaliani ni maoni kuwa mchakato mzima wa Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

"ACT Wazalendo tunasema mchakato wa mabadiliko ya tume ya uchaguzi na Katiba Mpya vianze sasa. Kuhusu katiba, mchakato mgumu zaidi ni kujenga mwafaka wa kitaifa.

“Bila mwafaka wa kitaifa, hakuna Katiba Mpya, tutaendelea kuvutana miaka nenda rudi bila kupata Katiba Mpya," kiongozi huyo alitoa angalizo.

Duni alisema ni lazima mazungumzo ya wadau wa Katiba Mpya yafanyike ili kupata mwafaka wa kitaifa kuhusu namna ya kuuendea mchakato wa Katiba Mpya.

Alisema kwa ujumla wanakubaliana kwenye maeneo mengi ya muda mfupi na wa kati yaliyopendekezwa na kikosi kazi cha Rais Samia.

“Tunakubaliana kuhusu kufunguliwa upesi kwa mikutano ya hadhara, kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Vyama vya Siasa na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Kwa hili la kuandikwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa, ninapenda kumkumbusha Mheshimiwa Rais kuhusu ahadi yake ya kuandikwa kwa sheria mpya kwenye Bunge hili la Bajeti ili nchi ipate sheria mpya ya vyama vya siasa tunapotimiza miaka 30 ya vyama vingi nchini," alisifu.

 

Kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi, Duni alisema ikiwapo nchini, itahakikisha Katiba Mpya yenye maoni ya wananchi inapatikana.

“Mara zote tumesema tutakuwa tunajidanganya iwapo tutakwenda kwenye kura ya maoni ya Katiba Mpya bila kuwa na tume huru. Tutapoteza tena mabilioni ya Watanzania iwapo tutataka katiba inayopendekezwa ipigiwe kura ya maoni ikisimamiwa na tume hii ya sasa ya uchaguzi,” alitahadharisha.

Alisema ili kupata Tume Huru ya Uchaguzi, ACT Wazalendo wanapendekeza kuandikwa upya kwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.

Duni alidai kuwa sheria ya sasa inaifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Tunataka tume itakayoweza kusimamia kura ya maoni ya Katiba Mpya na uchaguzi ujao kwa haki na kujiamini. Tumependekeza kuundwa kwa kamati huru ya uteuzi wa viongozi wa tume ambayo itajumuisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mwenyekiti na Jaji Mkuu wa Zanzibar kama Makamu Mwenyekiti,” alisema.

Duni alisema ACT-Wazalendo inapendekeza wajumbe wa kamati hiyo wawe: Rais wa Tanganyika Law Society (TLS), Zanzibar Law Society (ZLS), mtu mmoja atakayeteuliwa na mkuu wa shughuli za serikali bungeni na mwingine atakayeteuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Pia chama hicho kimependekeza endapo hakuna kambi rasmi ya upinzani bungeni, basi mtu huyo atolewe katika chombo kinachojumuisha vyama vyenye wabunge bungeni.

“Mtu mmoja kutoka asasi ya kitaifa ya masuala ya sheria na haki za binadamu Tanzania Bara na mwingine kutoka kwenye asasi kama hiyo Tanzania Zanzibar," alipendekeza.

Duni aliendelea: “Kwa vyovyote vile, angalau theluthi ya wajumbe wa kamati lazima wawe wanawake. Mbali na hilo, tunataka kuwe na sifa maalum za wajumbe wa tume zitakazowaongoza ili kuhakikisha wanaoteuliwa wanakuwa watu wenye weledi na wasiogemea upande wowote.”

Alikumbusha yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na kueleza kuwa ACT-Wazalendo inapambana kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwenye mazingira ya uhuru, haki na usawa.

Alisema bila Tume Huru ya Uchaguzi, Watanzania wataendelea kukata tamaa na itakuwa vigumu kuwashawishi kupiga kura.

00000000000

Habari Kubwa