ACT- Wazalendo kushiriki kikamilifu kumuaga Magufuli Zanzibar

21Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe Jumapili
ACT- Wazalendo kushiriki kikamilifu kumuaga Magufuli Zanzibar

CHAMA cha ACT- Wazalendo kimewataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi siku ya Jumanne Machi 23, 2021 katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja, Zanzibar kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga mjini humo, Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa chama hicho, Salim Bimani, amesema kuwa msiba huo ni mzito kwa wananchi wote na Taifa, hivyo wanatakiwa kushiriki kikamilifu.

“Tumepata msiba mkubwa na mzito kuondokewa na kiongozi mkubwa na shupavu, wito wangu kwa wanachama na wananchi wote tujitokeze kwa wingi kuaga kama ratiba inavyosema.”

“Tuwepo katika njia ambapo mwili utapita na kisha kushiriki katika Uwanja wa Amaan, sisi viongozi wa chama tupo mstari wa mbele na tutashiriki kikamilifu mwanzo hadi mwisho,” amesema Bimani

Bimani amesema kesho Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Juma Haji Duni,  ataongoza jopo la viongozi wa chama hicho kusaini kitabu cha maombolezo katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni mjini Unguja na baada ya hapo watakwenda katika Ofisi Kuu za CCM  Kisiwandui kuwapa pole viongozi wa chama hicho tawala na kusaini kitabu cha maombolezo.

Habari Kubwa