ACT-Wazalendo waunda timu kufatilia janga la corona

07Apr 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
ACT-Wazalendo waunda timu kufatilia janga la corona

Chama cha ACT Wazalendo kimeunda timu ya ufuatiliaji wa ugonjwa wa corona ili kufuatilia shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu imesema timu hiyo itaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Juma Duni Haji ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Afya Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara  Dorothy Semu ambaye pia ameelezwa kuwa aliwahi kufanya kazi katika Wizara ya Afya nchini.

“Kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona (COVID-19) na madhara yake makubwa kwa Taifa na kutokana na umuhimu wa uratibu wa suala hili Kiongozi wa ACT Wazalendo ,Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Taifa wa chama Maalim Seif  Sharif Hamad wameunda timu ya ufuatiliaji wa masuala ya COVID-19” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Wengine waliowekwa katika timu hiyo ni Janeth  Fusi ,Salim Bimani ,Pavu Abdallah ,Janeth Rithe  Mbarala Maharagande , Issa Kheri na Seif  Abalhassan.

Akieleza malengo hasa ya timu hiyo Katibu Mkuu huyo amesema kuwa ni kufuatilia kwa karibu shughuli za Serikali katika suala la corona na kutoa ushauri katika chama hicho kuhusu namna bora ya kuhamasisha umma kuhusu kuratibu ugonjwa huo na mikakati ya chama kukabiliana nao.

Habari Kubwa