ACT-Wazalendo yalilia chakula

20Feb 2017
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
ACT-Wazalendo yalilia chakula

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeiomba serikali kuangalia upya namna ya kuwasaidia wananchi wenye upungufu wa chakula pamoja na kutangaza rasmi janga la ukame nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii wa chama hicho, Janeth Rithe, alisema kutokana na upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini, zipo baadhi ya wilaya zenye upungufu wa chakula ambazo pia zinakabiliwa na ukame.

Alisema kama ambavyo serikali imeonyesha moyo wa kushughulikia matatizo mengine, ni vema pia isilifumbie macho suala hilo.

“Sisi kama chama, tumefanya utafiti na kubaini kuwapo kwa upungufu wa chakula karibu wilaya 50," alisema Janeth na kueleza "lengo letu tunaomba serikali isilifumbie macho hili."

"Kama amabavyo inashughulikia matatizo mengine, iliangalie na hili.

“Na pia tunaiomba itangaze uwapo wa ukame nchini, kwa sababu maeneo mengi ya nchi ambayo tumeyafanyia utafiti tumebaini yana ukame."

Alisema pamoja na kutangaza, serikali ni lazima iangalie namna ya kuwapa wananchi elimu ya kilimo cha umwagiliaji na si kutegemea mvua pekee kama sasa.

Pia alisema ni vema serikali ikaangalia namna ya kujenga maghala ya kutosha ya kuhifadhia chakula na kuliomba Bunge kuongeza bajeti katika mfuko wa hifadhi ya chakula ya taifa.

BEI YA VYAKULA
Akizungumzia mfumuko wa bei ya vyakula, Rithe alisema ni jambo la kushangaza kuona hata katika mikoa ambayo imekuwa ikitegemewa kulisha nchi, nayo inakabiliwa na upungufu wa chakula na mfumuko mkubwa wa bei ya vyakula.

“Ukienda hata mkoa wa Morogoro ambao ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa kulisha nchi pale inapotokea njaa, nao una upungufu wa chakula na hivi sasa bei za vyakula katika mkoa huo ziko juu," alisema.

"Wananchi wenye kipato cha chini wanashindwa kumudu.”

Alitaja mikoa mingine ambayo bei ya vyakula imepanda, hususani unga wa mahindi na maharage kuwa ni pamoja na Arusha, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Mwanza, Morogoro na Tabora.

Alisema katika kupambana na hali ya ukame, ni vema serikali ikawekeza zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ikiwamo kupunguza bajeti ya ruzuku.

Hata hivyo, Januari 16 serikali ilisema licha ya baadhi ya maeneo nchini kutopata mvua za kutosha na kusababisha ukame, lakini chakula kipo cha kutosha mpaka msimu ujao wa kilimo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la ATCL kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Majaliwa alisema mwaka jana, nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu, ambapo baadhi ya wabunge na wafanyabiashara, waliomba kibali cha serikali ili waweze kuuza nje ya nchi. Alisema serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha.

Majaliwa alifafanua kuwa baada ya kutoa kibali hicho, tani milioni 1.5, ziliuzwa nje ya nchi na serikali ilisitisha uendelezaji wa kuuzwa kwa chakula hicho baada ya kufika tani hizo.

Alisema tani milioni 1.5, zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba, ambapo hivi sasa wameruhusu kiuzwe hapa nchini ili kupunguza gharama ya bei sokoni.

Habari Kubwa